Arsenal yaendeleza matokeo duni

Imebadilishwa: 5 Disemba, 2012 - Saa 11:20 GMT

Arsenal imekumbwa na matokeo duni sana katika mechi zake za hivi karibuni

Arsenal iliendeleza msusruru wa matokeo mabaya na kupoteza nafasi ya kumaliza katika kilele cha kundi B kwenye Ligi ya klabu bingwa barani Ulaya, baada ya kushindwa na Olympiakos, mjini Athens.

Upande huo wa Gunners uliofanya mabadiliko saba, ulianza vyema na Tomas Rosicky aliwapa bao la mapema kabla ya kipindi cha mapumziko.

Mkufunzi Arsene Wenger aliwaanzisha Marouane Chamakh, Francis Coquelin na Sebastien Squillaci, huku Jernade Meade, mwenye miaka 20 pekee, akianza mara ya kwanza kabisa kama mlinzi upande wa kushoto.

Vijana wengine watano chipukizi vilevile walitajwa katika kikosi cha Wenger.

Mabadiliko hayo yalionekana kuipatia Arsenal motisha iliyohitaji na mfumo huo wake wa 4-3-3 ulikuwa na makali katika safu ya mashambulizi.

Wachezaji Gervinho, Chamakh na Alex Oxlade-Chamberlain walikuwa na nafasi za mapema huku Aaron Ramsey akipoteza nafasi ya wazi mbele ya lango la Olympiakos.

Lakini Olympiakos ilisawazisha kupitia bao la karibu la Giannis Maniatis na kisha kuchukua uongozi kupitia mkwaju uliojipinda wa Kostas Mitroglou.

Arsenal tayari ilikuwa imefuzu kwa raundi ya 16 bora lakini ikaibuka ya pili katika kundi hilo la B. Hii ina maana kuwa huenda ikapatana na timu kama Barcelona, Paris Saint-Germain au Borussia Dortmund katika raundi ya 16 bora.

Licha ya kuwa huenda wakafurahishwa na kufuzu kuingia raundi ya 16 bora kwa msimu wa 13 mfululizo, Gunners sasa wameshinda mechi zao nne tuu kati ya 13 katika mashindano yote msimu huu.

Hii ilikuwa mara ya tatu katika miaka minne kwa Arsenal kushindwa na Olympiakos katika mechi za mwisho za makundi, na kiwango cha mchezo wa wachezaji wa klabu hiyo itamfanya kocha Arsene Wenger kukuna kichwa chake.

Macho yote sasa yanaangaziwa mechi ya ugenini ya Jumamosi dhidi ya West Brom katika ligi kuu nchini Uingereza, ambapo Arsenal inashikilia nafasi ya 10, ikiwa na pointi 21 kutokana na mechi 15.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.