Mikel aongezewa miaka mitano

Imebadilishwa: 5 Disemba, 2012 - Saa 18:40 GMT

Kiungo cha kati wa Chelsea, John Obi Mikel, ametia saini mkataba mpya wa miaka mitando kuendelea kusakata gozi Stamford Bridge, hadi mwaka 2017.

John Obi Mikel

Mikel kuendelea kucheza Stamford Bridge kwa muda wa miaka mitano

Klabu hicho cha ligi kuu ya Premier kilitangaza habari hizo siku ya Jumatano.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Nigeria alijiunga na Chelsea akiwa kijana mwenye umri wa miaka 19 mwaka 2006.

Hadi wakati huu ameichezea Chelsea jumla ya mechi 261, na kushuhudia ushindi mara nyingi; ubingwa wa klabu bingwa barani Ulaya, medali nne za Kombe la FA, ushindi mmoja wa ligi kuu ya Premier, na Kombe la Ligi.

"Nimepata ushindi nikiwa na Chelsea karibu katika mashindano yote makubwa, na miaka niliyoichezea Chelsea ni maalum sana kwangu, nikitwaa ushindi na wachezaji nyota kama Didier Drogba, John Terry na Frank Lampard ambao wameichezea Chelsea kwa muda mrefu," Mikel alielezea katika taarifa katika tovuti ya klabu (www.chelseafc.com).

"Ushindi wa klabu bingwa msimu uliopita ulikuwa muhimu hata zaidi," aliongezea "na natumaini miaka hiyo mitano ijayo italeta ufanisi zaidi na kuniwezesha kushinda vikombe zaidi nikiwa na wachezaji wapya waliojiunga na timu."


Awali, Mikel alikuwa kiungo cha kati aliyejizatiti zaidi katika kushambulia, lakini chini ya meneja wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho, akawa ana jukumu la ulinzi.

"Nikiwa umri wa miaka 25 nadhani ninafikia kilele changu, lakini kama mchezaji, ninapenda kujiimarisha kila kukicha, na nadhani nina nafasi hiyo. Ningelipenda kujifunza zaidi kutoka kwa wachezaji na vile vile meneja", aliongezea.

Mikel alijipata katika utata, kwa kumlaumu mwamuzi Mark Clattenburg kwa kutumia lugha isiyofaa katika mechi, wakipambana na Manchester United mwezi Oktoba.

Hata hivyo utafiti uliofanywa na idara ya polisi ya Metropolitan na vile vile chama cha soka cha FA ilithibitishwa kwamba hamna ushahidi wa kutosha kumfungulia kesi Clattenburg.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.