Messi avunja rekodi

Imebadilishwa: 10 Disemba, 2012 - Saa 13:35 GMT
Lionel Messi

Lionel Messi akisherehekea bao lake

Mshambulizi matata wa Barcelona Lionel Messi, ameweka rekodi mpya kwa kufunga bao lake la 86 mwaka huu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, kutoka Argentina, alivunja rekodi iliyowekwa na Gerd Mueller ya kufunga magoli 85 mwaka wa 1972 na kuweka rekodi mpya, ambayo pia inajumuisha idadi ya magoli aliyoyafungwa na timu yake ya taifa na klabu ya Barcelona.

Messi alivunja rekodi hiyo baada ya kufunga magoli mawili wakati wa mechi yao dhidi ya Real Betis siku ya Jumapili, ambayo Barcelona ishinda kwa magoli mawili kwa moja.

Baada ya dakika kumi na sita za mechi hiyo Messi alifunga bao la kwanza na kusawazisha rekodi hiyo, kabla ya kuongeza la pili kunako dakika ya 25 na kuweka rekodi mpya.

Messi abebwa kwa machela

Lionel Messi

Lionel Messi wakati alipojeruhiwa

Juhudi za mchezaji huyo za kuvunja rekodi hiyo iliyowekwa na Mjerumani Mueller, zilionekana kuambulia patupu, baada ya mchezaji huyo kujeruhiwa na kubebwa kwa machela wakati wa mechi yao kuwania kombe la klabu bingwa barani Ulaya dhidi ya Benfica siku ya Jumatano.

Ili kuvunja rekodi hiyo, Messi ameifungia Bercelona jumla ya magoli 74 na 12 kwa timu ya taifa ya Argentina.

Hata hivyo Messi angali ana nafasi ya kuweka rekodi mpya kwa kuwa mechi mbili zimesalia kabla ya mwaka huu kumalizika.

Mueller aliifungia klabu yake ya Beyern Munich magoli 72 na timu yake ya taifa ya Ujerumani ya Magharibi magoli 13, mwaka wa 1972 akiwa na umri wa miaka 27.

Messi sasa anatarajiwa kutwaa taji la mchezaji bora wa soka mwaka huu kwa mwaka wa nne mfululizo lakini anakabiliwa na upinzani mkali kutokwa kwa mchezaji mwenzake wa Barcelona, Andres Iniesta na Christiano Ronaldo wa Real Madrid.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.