Wachezaji wa Zanzibar wapigwa marufuku

Imebadilishwa: 12 Disemba, 2012 - Saa 16:25 GMT
Timu ya soka ya Zanzibar

Timu ya soka ya Zanzibar

Shirikisho la mchezo wa Soka visiwani Zanzibar,ZFA limechukua uamuzi ambao umewashngaza sana mashabiki wengi wa soka, visiwani humo, nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

Kwa mujibu wa ripoti maafisa wakuu wa ZFA wamewapiga marufuku wachezaji wake wote walioshiriki katika michuano ya kuwania kombe CECAFA Senior Challenge, iliyokamilika nchini Uganda, kutoshiriki katika mechi yoyote popote duniani kwa muda usiojulikana.

Aidha ZFA limeamua kuvunja timu ya taifa maarufu kama Zanzibar Heroes, licha ya kuwa timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya tatu katika michuano hiyo ya CECAFA.

Baadhi ya wachezaji hao waliopigwa marufuku ni pamoja na nyota na naodha wa Yanga, Nadir Haroub.

Kwa nini ZFA ilichukua hatua hiyo?

Nadir Haroub

Nadir Haroub naodha wa Yanga

Wachezaji hao wanakabiliwa na tuhuma za utovu wa nidhamu.

Akitoa tangazo hilo, katika makao makuu ya shirikisho hilo, makamu wa rais wa ZFA Alhaj Haji Ameir, alisema wanachama wote wa kamati kuu ya ZFA kwa kauli moja waliafikiana kuhusu hatua hiyo, ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine.

Kamati hiyo ya ZFA iliitisha kikao cha dharura, baada ya wachezaji hao wa Zanzibar Heroes, kugawana fedha walizoshinda wakati wa michuano hiyo ya CECAFA.

Zanzibar ilimaliza katika nafasi ya tatu na hivyo kujishinda dola elfu Kumi za Kimarekani.

Ripoti zinasema fedha hizo ziligawanywa na wachezaji hao kama njia moja ya kuwasilisha malalamishi yao kwa ZFA kuhusiana na jinsi wao wanavyoshughulikiwa wakiwa kambini.

Inadaiwa kuwa wachezaji hao waliamua kugawana fedha hizo kwa madai kuwa wamekuwa wakidhulumiwa fedha zao na ZFA.
Baadhi yao wanasema ZFA huwa na mazoea ya kuchukua hela zote wanazoshinda bila hata kuwapa chochote ili hali wao ndio waliofanya kazi zaidi.

Kinyume na matarajio ya wengi kocha mkuu wa Zanzibar Heroes, Salum Bausi ambaye kujiuzulu baada ya mashindano hayo ya CECAFA, amewashangaza wengi kwa kuunga mkono, uamuzi huo akisema wachezaji hao wameharibu sifa ya Zanzibar.

Hata hivyo kuna baadhi ya wachezaji walioamua kurejesha fedha walizopewa kwa shirikisho hilo na ZFA haijatoa orodha yao.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.