Van Persie ana bahati kuwa hai

Imebadilishwa: 23 Disemba, 2012 - Saa 18:12 GMT
Robin Van Persie

Meneja wa Man Utd anasema mshambulizi wake angeliweza kuuawa kwa kutandikwa kichwa kwa mpira

Sir Alex Ferguson, meneja wa Manchester United, amesema inafaa chama cha soka cha England cha FA kumchukulia hatua Ashley Williams, mlinzi wa Swansea, kwa kudai mchezaji huyo alikuwa nusra asababishe 'kifo' cha Robin van Persie katika mchezo wa Jumapili uliokwisha kwa sare ya 1-1 katika uwanja wa Liberty.

Van Persie aligongwa kisogo kwa mpira wakati Williams, akiwa hatua chache mno, aliondosha mpira hatarini, huku tayari mchezaji huyo wa Manchester United akiwa chini baada ya kuchezewa vibaya na Nathan Dyer, karibu na lango la wenyeji Swansea, katika dakika ya 75.

Hata hivyo, mchezaji huyo wa kimataifa wa Wales haikuonekana kama kwa maksudi alitaka kumchanganya Van Persie katika kuondosha mpira, lakini mwamuzi tayari alikuwa amepuliza firimbi.

Mshambulizi huyo wa Man United alipandwa na gadhabu, na wachezaji kadha kuingilia ubishi huo, huku mwamuzi Michael Oliver akiwaonyesha wahusika wote wawili walioanzisha fujo, Williams na Van Persie, kadi za manjano.

Ferguson alilalamika vikali baada ya mechi, akisema Williams alikuwa na nia ya kumjeruhi Van Persie, na kuelezea kwamba mshambulizi wake alinusurika kuvunjwa shingo.

''Katika hali aliyojipata Van Persie ni wazi kwamba pengine angeliuawa,'' Ferguson alisema alipokuwa akizungumza katika matangazo ya kituo cha Sky Sports News.

''Chama cha FA lazima kichunguze tukio hili, licha ya kwamba ameonyeshwa kadi ya njano. Inafaa apigwe marufuku asicheze kwa muda mrefu, kwa sababu hilo ni tukio la hatari mno ambalo sijawahi kuliona katika soka kwa muda wa miaka mingi.''

''Ilikuwa ni kwa maksudi kabisa. Kipenga kilikuwa kimepulizwa, mchezo umesimama, na amefanya hivyo mbele ya mwamuzi. Angeliweza kusababisha kifo cha mchezaji huyoe.''

''Ilikuwa ni kitendo cha aibu, na apigwe marufuku kwa muda mrefu.''

Meneja wa Swansea Michael Laudrup alionekana kucheka alipoelezwa juu ya matamshi ya Ferguson.

Alisema: ''Sikuona hasa kilichofanyika wakati huo, kwani wachezaji wengi walimzingira, lakini baadaye nilitizama yaliyotokea.''

''Sidhani hasa Ferguson anamaanisha kwa hakika kweli mchezaji huyo angelikufa.''

''Mambo hutokea katika mchezo, na nina hakika Ashley na Van Persie wamepeana mikono baada ya kipenga cha mwisho, na maisha kusonga mbele.''

Nahodha huyo wa Wales alisema: ''Nilijaribu kuondoa mpira, na ulimtandika kichwa.''

''Ilikuwa dhahiri alikasirishwa na jambo hilo.''

Ugomvi huo ulipunguza burudani ya kufurahisha, wakati United walipokosa nafasi ya kuwa kileleni kwa kukosa ushindi na kuwawezesha kuongoza ligi kwa kuwa mbele kwa pointi sita zaidi.

Patrice Evra aliwasaidia wageni kuongoza kwa kufunga kwa kichwa, baada ya kupata mpira kutoka kwa Van Persie katika dakika ya 16, lakini Michu akapata bao la kusawazisha, na likiwa bao lake la 13 katika ligi kuu ya Premier ya England msimu huu.

Meneja Laudrup alisema: ''Ilikuwa ni pointi muhimu kwa klabu na wachezaji. Nilisikia kwamba msimu uliopita United waliheshimiwa sana, lakini leo mambo hayakuwa hivyo.''

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.