Kocha asema Chipolopolo imejiandaa vyema

Imebadilishwa: 16 Januari, 2013 - Saa 15:03 GMT

Wachezaji wa Zambia

Kocha wa Zambia Herve Renard, amesema ameridhika na jinsi kikosi chake kimejiandaa kwa fainali za kombe la mataifa ya Afrika.

Kocha huyo wa Zambia, amesema kuwa kikosi chake kiko imara kuliko ilivyokuwa mwaka uliopita, huku wakijiandaa kutetea kombe hilo nchini Afrika Kusini.

Chipolopolo inaanza kampeini yake tarehe 21 Januari dhidi ya Ethiopia, baada ya kushindwa mechi tatu na kutoka sara moja wakati wa mechi zao za kirafiki.

Licha ya kipigo hicho Renard, ambaye aliongoza Zambia kushinda kombe hilo kwa mara ya kwanza, mwaka uliopita, amesema ameridhika na maandalizi yake.

''Naamini kuwa tuko imara kuliko tulivyokuwa mwaka uliopita wakati kama huu'' Alisema kocha huyo.

Renard amesema mwaka uliopita, kabla ya kuanza kwa fainali hizo alikuwa na wasi wasi kwa kuwa maandalizi yao yaliyokuwa duni sana.

Kocha wa Zambia

''Lakini kinyume na matarajio yetu, tulifanya vyema na kushinda kombe hilo'' Aliongeza kocha huyo.

Zambia ilitoka sare ya kutofungana bao lolote na Morocco, katika mechi ya kirafiki mjini Johannesburg, wiki iliyopita na kusitisha rekodi ya timu hiyo ya kushindwa.

Kabla ya mechi hiyo Zambia ilishindwa na Angola, Saudi Arabia na Tanzania.

Lakini Renard, licha ya matokeo hayo duni, amesema hana wasi wasi kuhusu kikosi chake.

Zambia inacheza Ethiopia katika mechi yake ya kwanza kisha Nigeria na Burkina Faso katika kundi C.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.