Armstrong: Kwa nini adhabu ya kifo?

Imebadilishwa: 19 Januari, 2013 - Saa 10:54 GMT
Lance Armstrong

Asema haelewi kwa nini amekabidhiwa 'hukumu ya kifo'

Mwendeshaji baiskeli Lance Armstrong ameelezea kushangaa kwa kukabidhiwa adhabu ya maisha ya kutoshiriki katika michezo, ilhali wanamichezo wenzake wamekuwa wakipigwa marufuku ya miezi sita tu.

Katika sehemu ya pili ya mazungumzo yake na Oprah Winfrey, mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 41 alisema: "Ninastahili kuadhibiwa. Lakini sidhani ninastahili hukumu ya kifo.

"Ningelitamani sana kupata nafasi ya kushindana, lakini hiyo sio sababu ya yale ninayoyafanya."

Kwa usiku wa pili, mazungumzo yake na Winfrey, mwenye umri wa miak 58, yalipeperushwa katika muda ambao watazamaji wengi walipata fursa ya kutizama televisheni, na yalionekana kote duniani kupitia tovuti yake.

Mazungumzo hayo yalikuwa hewani kipitia kituo cha Winfrey cha televisheni nchini Marekani, OWN, yaani Oprah Winfrey Network.

Katika sehemu ya kwanza ya mazungumzo yao, Mmarekani Armstrong hatimaye alikiri kutumia dawa za kuongezea nguvu michezoni zilizopigwa marufuku, baada ya kukanusha kwa muda wa miaka mingi, na huku akiibuka bingwa mara saba wa mashindano ya baiskeli ya Tour de France.

Katika sehemu ya pili ya mazungumzo, Armstrong alijizuia kulia, huku akielezea namna familia yake imeathirika kutokana na vitendo vyake.

Kuhusu kutamani kurudi katika mashindano ya Tour de France, Armstrong alielezea hana matumaini ya hayo kufanyika, lakini akaongezea: “Ikiwa unaninuliza kama ningelipenda kushindana tena, jibu ni, ndio, mimi ni mshindani kweli. Hayo nimeyafanya katika maisha yangu yote. Ningelipenda kushindana na wengine.

“Kuna mambo mengi ambayo siwezi kuyafanya kutokana na kupigwa marufuku. Lakini kama kuna nafasi, ningelipenda kushiriki katika mbio ya marathon ya Chicago, nikiwa na umri wa miaka 50. Ndio.”

“Unapoitaja adhabu niliyokabidhiwa….nimepata hukumu ya kifo, ikimaanisha siwezi kushindana. Sisemi nimeonewa, lakini ni adhabu tofauti.”

Armstrong alisema kwa “ubinafsi” angelipenda marufuku hiyo ya maisha iondolewe. “Lakini kwa hakika, sidhani hilo litafanyika, na itanibidi kuishi kwa kuikubali hukumu hiyo.”

Tarehe 17 Oktoba, mwaka jana, mara tu baada ya habari kuchapishwa kwama alikuwa ni mtu laghai, siku sita baadaye wadhamini wake wa michezo walisitisha udhaimini wao, ikiwa ni pamoja na makampuni makubwa kama Nike, watengezaji baiskeli Trek, na kampuni ya kutengeneza pombe ya Budweiser, Anheuser-Busch.

Wakati huo ilidhaniwa Armstrong alipata hasara ya dola milioni 30, lakini akizungumza na Winfrey, alisema ilikuwa ni hasara ya dola milioni 75 kwa siku.

Zaidi ya watu milioni 4.3 nchini Marekani walitizama sehemu ya kwanza ya mazungumzo hayo katika televisheni ya Winfrey, OWN.

Wengine 600,000 nchini humo walitizama moja kwa moja kupitia tovuti yake ya Oprah.com.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.