Miamba wa Maghreb Tunisia kuvaana na Algeria

Imebadilishwa: 21 Januari, 2013 - Saa 15:16 GMT

Mchezaji wa Tunisia

Tunisia inatarajiwa kuanza kutupa karata yake ya kwanza katika michuano ya fainali za Kombe la Afrika, kundi D, itakapokabiliana na Algeria, Jumatano, nchini Afrika Kusini.

Tunisia moja ya timu zilizopata mafanikio makubwa katika michuano ya Afrika na Kombe la Dunia inamtegemea mchezaji kiungo Youssef Msakni, anayejulikana kama Little Mozart, kusukuma mashambulio katika lango la adui.

Tunisia inawania taji la pili la michuano ya Afcon baada ya mwaka 2004 kutawazwa mabingwa walipoitoa Morocco kwa magoli 2-1 katika fainali.

Tunisia walikuwa wenyeji wa michuano hiyo.

Kocha Sami Trabelsi, ambaye aliingia kwa kishindo mwaka 2011 kwa kutwaa ubingwa wa mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani, katika mashindano yaliyofanyika nchini Sudan, amepanga malengo ya kufika robo fainali katika michuano hiyo.

"Hili halina ubishi kuwa tuko katika kundi gumu kuliko yote manne ya kwanza, lakini hatulalamiki kujikuta katika kundi hili," amesema kocha Trabelsi.

Mashabiki wa Algeria

"Wachezaji wangu kwa kweli wanajibidiisha na ninaamini tutafika mbali- huenda hatua ya mwisho ya kuamua nani bingwa," amesema, akirejelea fainali za mwaka 1996, wakati Tunisia ilipofungwa na Afrika Kusini katika fainali mjini Johannesburg.

Kwa upande wa kikosi cha Algeria, timu nyingine ngumu kutoka Afrika ya Kaskazini, wakijivunia mafanikio kama vile kufikia hatua ya nusu fainali ya michuano ya Afrika mwaka 2010.

Kama ilivyo Tunisia, Algeria nayo imeweza kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010, baada ya miaka 24 kutoonekana katika michuano hiyo mikubwa duniani.

Mafanikio haya yametokana na sera ya kuwaruhusu wachezaji wenye uraia wa mataifa mawili kuchezea nchi hiyo. Miongoni mwao ni wachezaji Madjid Bougherra na Mehdi Lacen.

Lakini kikosi kilichopo Afrika Kusini kina sura mpya kama mlinda mlango Faouzi Chaouchi.

Vijana wengi ndio wanaunda kikosi cha Algeria. Sofiane Feghouli nyota wa Valencia ya Hispania atashirikiana na mshambuliaji kiungo mwenzake Foued Kadir kutaka kutikisa nyavu za Tunisia.

"Kikosi changu hakina uzoefu wa michuano mikubwa kama hii, lakini wakiwa wamejawa na shauku ya kufanya vizuri.

Japokuwa najiamini, halitakuwa jambo kubwa la kushangaza iwapo tutatolewa katika hatua ya makundi," amesema kocha Vahid Halilhodzic wa Algeria.

"kama tutafika robo fainali, huwezi kujua kinachoweza kutokea, lakini tutatakiwa kufika hapo kwanza na kufanya hivyo kunaanza kwa kupata matokeo mazuri tutakapocheza dhidi ya Tunisia."

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.