Ivory Coast 3 Tunisia 0

Imebadilishwa: 26 Januari, 2013 - Saa 15:52 GMT

Nahodha wa Ivory Coast Didier Drogba

Ivory Coast inakaribia kufuzu kwa robo fainail ya michuano ya kuwania kombe la mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Afrika Kusini katika kundi D.

Ivory Coast imeididimiza Tunisia katika mechi yao ya pili ya kundi D kwa magoli 3-0.

Ivory Coast ilipata bao lake la kwanza kunako dakika ya 21 kupitia kwa nyota wake Gervinho.

Bao la pili limefungwa na Yahya Toure kipindi cha pili dakika ya 85, huku bao la tatu likifungwa na Didier Yakonan katika dakika ya 88.

Tunisia ambayo kipindi cha pili ilionyesha uhai na kufanya mashambulio kadhaa, ilijikuta ikiadhibiwa na wachezaji hao nyota wazoefu wa michuano ya kimataifa.

Matokeo hayo sasa yanamaanisha kuwa Ivory Coast inanukia kufuzu kwa robo fainali ya mashindano hayo.

Ivory Coast itafuzu kwa robo fainali ikiwa itatoka sare ya aina yoyote katika mechi yao ya mwisho na Algeria ambapo itakuwa imezoa alama saba.

Hata hivyo Ivory Coast inaweza kuyaaga mashindano hayo ikiwa Tunisia na Algeria watamaliza kundi hilo na alama sita na kufunga idadi kubwa ya magoli kuliko Ivory Coast.

Kufikia sasa Ivory Coast imefunga magoli matano na kufungwa goli moja.

Ivory Coast sasa ina alama sita, Tunisia nayo inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi tatu, huku Algeria na Togo ambazo zitapambana muda mfupi ujao zikiwa hazina pointi baada ya kupoteza mechi zao za kwanza.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.