Burkina Faso yafuzu kwa nusu fainali

Image caption Mchezaji wa Burkina Faso

Burkina Faso hatimaye imekuwa timu ya nne kufuzun kwa nusu fainali ya kuwania kombe la mataifa ya Afrika baada ya kuilaza Togo kwa bao moja kwa bila, katika mechi ya mwisho ya robo fainali.

Licha ya Togo kupigiwa upato kushinda, mechi hiyo sawa na ilivyokuwa katika robo fainali ya kwanza dhidi ya Ivory Coast na Nigeria, Burkina Faso ilifuzu kwa nusu fainali hizo.

Togo itajilaumu sana kwa kupoteza mechi hiyo, baada ya wachezaji wake kupoteza nafasi nyingi sana za kufunga wakati wa mechi hiyo.

Baada ya dakika tisini za kawaida kumalizika, hakuna timu iliyokuwa imeona lango la mwenzie hatua iliyopelekea mechi hiyo, kuongezwa muda zaidi.

Kunako dakika ya 105 Burkina Faso hatimae ikapata goli kupitia mchezaji wake Jonathan Pitroipa.

Pitroipa alifunga bao hilo kwa kichwa kufuatia mpira wa kona.

Burkina Faso sasa itacheza na Ghana katika nusu fainali ya pili siku ya Jumatano mwendo wa saa mbili na nusu majira ya Afrika Mashariki.

Nusu Fainali ya kwanza itakuwa kati ya Nigeria na Mali.

Kwa mwaka mwingine tena timu zilizosalia kwenye mashindano hayo, zinatoka Afrika Magharibi baada ya timu nyingine kutoka maeneo ya Kaskazini, Mashariki na Kusini kubanduliwa nje ya michuano hiyo.