Nigeria wazidi kung'ara,watinga fainali

Image caption Wachezaji wa Nigeria

Nigeria yatinga fainali baada ya kuicharaza Mali magoli 4-1 katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali za Kombe la Afrika.

Elderson Echiejile aliifungia magoli mawili ya kwanza katika dakika ya 25 na 30 ya mchezo.

Goli la tatu lilifungwa na Emenike katika dakika ya 44 baada ya mpira aliopiga kumgonga Momo Sissoko wa Mali.

Hadi mapumziko Nigeria ilikuwa ikiongoza kwa 3-0.

Ahmed Musa alizidi kuleta majonzi kwa mashabiki wa Mali alipofunga bao la nne katika 60.

Mali ilizidi kusaka bao, katika dakika ya 70 Cheikh Diarra aliifungia timu yake bao la kufutia machozi.

Nigeria kuingia nusu fainali waliwabwaga Ivory Coast 2-1, timu ambayo ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kucheza fainali kutokana na ubora wa wachezaji wake.

Nayo Mali iliwatoa wenyeji wa mashindano Afrika Kusini kwa njia ya mikwaju ya penalti 3-1 baada ya timu hizo kucheza dakika 120 zikiwa zimefungana goli 1-1.

Timu nyingine katika nusu fainali za Afcon ni Ghana itakayokwaruzana na Burkina Faso. Ghana waliitoa Cape Verde katika hatua ya robo fainali kwa magoli 2-0, huku Burkina Faso wakiifunga Togo kwa goli 1-0.

Sasa Nigeria inamsubiri mshindi kati ya Ghana na Burkina Faso zinazocheza mchezo wa pili wa nusu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2013.