Ghana 1 Mali 3

Image caption Kikosi cha Mali

Mali yatwaa nafasi ya tatu katika michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2013 zinazokamilika kesho, Jumapili nchini Afrika Kusini.

Mali ilipata goli la kuongoza katika kipindi cha kwanza katika dakika ya 21 likifungwa na Mahamadou. Hadi mapumziko Mali ilikuwa ikiongoza kwa hilo goli.

Kipindi cha pili kilianza kwa Mali tena kufunga katika dakika ya 48, mfungaji akiwa ni Seydou Keita.

Ghana ilijitutumua na kupata bao la kufutia machozi katika kipindi hicho cha pili. Hata hivyo furaha yao haikudumu sana baada ya kuchapwa goli lingine la tatu na la ushindi kwa Mali.

Image caption Assamoah Gyan mchezaji wa Ghana

Matokeo haya yanaendeleza ubabe wa Mali dhidi ya Ghana, ambapo mwaka jana katika mchezo kama huo wa kutafuta mshindi wa tatu wa michuano ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika 2012, Mali iliichapa Ghana 2-0.

Ni mwaka mmoja kamili, wakati Ghana na Mali zilipokuwa zikijiandaa kucheza mechi ya kusaka nafasi ya tatu baada ya timu zote mbili kupoteza matumaini ya ubingwa zilipotolewa katika nusu fainali za michuano ya kombe la Afrika za mwaka 2012.

Mchezo huu, unatoa fursa ya kuhitimisha michuano hiyo ambapo bingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mwaka 2013 atapatikana, ukizikutanisha Nigeria na Burkina Faso hapo keho.

Ghana na Mali baada ya kukosa kombe hili, jitihada zinaelekezwa katika kutafuta nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2014 zitakazofanyika nchini Brazil.