Arsenal hatimaye yafuta aibu kwa ushindi

Image caption Santi Carzola

Arsenal imeilaza Aston Villa kwa mabao mawili kwa moja katika mechi ya ligi kuu iliyochezwa katika uwanja wa Emirate.

Mabao mawili ya Mhispania Santiago Carzola, yalitosha kuifanya Arsenal kuwa kwenye nafasi ya tano, wakiwa na tofauti ya point moja na majirani zao Tottenham ambao wao watashuka uwanjani siku ya Jumatatu kucheza na West Ham United, kwenye uwanja wa Upton Park.

Aston Vila, ambao walijitahidi kuhimili mikiki mikiki ya Arsenal, watajilaumu wenyewe kwa kupoteza nafasi kadhaa na kuruhusu bao la pili na ushindi kwa Arsenal dakika za lala salama.

Kwingineko,magoli mawili ya Romelu Lukaku, yalitosha kuididimiza Sunderland na kuifanya West Brom, kuibuka na ushindi wao wa kwanza kwenye uwanja wa nyumbani toka mwezi Desemba mwaka jana.

Image caption Romelu Lukaku akisherehekea bao lake

Hii ilikuwa ni baada ya ushindi wa mabao mawili kwa moja katika mchezo uliokuwa mkali na wa kusisimua.

West Brom walianza kupata bao lao kwa njia ya penati baada ya Craig, Gardner kuunawa mpira kwenye eneo la hatari,penati ambayo ilizamishwa nyavuni na Lukaku ambaye aliongeza bao la pili kufanya juhudi binafsi za kuuchukua pasi ya kizembe iliyorudishwa kwa kipa na beki Titus Bramble na kufanya West Brom kuwa mbele kwa mabao mawili kwa bila.

Lakini dakika kumi kabla mpira haujamalizika, Stephane Sessegnon alipiga shuti kali mita 12 kutoka lango la West Brom na kuipatia Sunderland bao la kufutia machozi.

Katika mchezo mwingine,Bao la dakika za lala salama la Grant Holt wa Norwich lilitosha kuipa ushindi wa kwanza baada ya michezo kumi ya ligi kuu soka nchini England timu hiyo dhidi ya Everton.

Norwich ambao walikuwa nyuma kwa bao moja kwa bila,bao la Leon Osman hadi kipindi cha kwanza kinamalizika,lakini iliwachukua dakika sita za mwisho kusawazisha na kupachika bao la pili na ushindi katika mchezo huo ambao ulionekana kuwashangaza mashabiki wa Evrton ambao walikuwa na imani ya ushindi katika mchezo huo.