Mwenyekiti mpya FA atajwa

mwenyekiti FA
Image caption Mwenyekiti wa FA,David Bernstein

Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa shirika la habari la BBC,Greg Dyke anatarajiwa kutangazwa kuwa mwenyekiti mpya wa chama cha soka nchini England,FA kuchukua nafasi ya David Bernstein.

Dyke ambaye itamlazimu kujiuzulu nafasi yake ya sasa mwenyekiti wa klabu ya Brentford,atachukua nafasi ya David Bernstein hapo mwezi Julai baada ya kuthibitishwa na baraza la FA.

"Najisikia ni mwenye furaha sana kutajwa kama mwenyekiti ajaye wa FA,Mpira wa miguu umekuwa mchezo wenye nafasi kubwa katika maisha yangu," Alisema Dyke.

Mwenyekiti wa sasa wa FA bwana David Bernstein mwenye umri wa miaka 69,aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa caham cha soka nchini England mapema mwaka 2010,atalazimika kuachia madaraka hayo atakapofikisha umri wa miaka 70 kama sheria ya chombo hicho chenye dhamana ya soka nchini Uingereza kinavyotamka kuwa,mwenyekiti wa chama hicho atatakiwa kutokuwa na umri wa zaidi ya miaka 70.

Kwa upande wake Greg Dyke mwenye umri wa miaka 65,alipata kuwa Mkurugenzi mtendaji wa BBC kuanzia mwaka 2000 mpaka 2004 na kwa sasa ni mwenyekiti wa taasisi ya filamu ya Uingereza na pia ni mwenyekiti wa klabu ya Brentford.

Amewahi kuwa Mkurugenzi wa klabu ya Manchester United kwa miaka miwili kuanzia mwaka 1997 mpaka 1999 na pia kuwa Mwenyekiti asiye mtendaji kwa miaka saba kwenye ligi daraja la kwanza nchini Uingereza kupitia klabu ya Brentford.

Moja ya changamoto kubwa ambazo atakuwa akizikabili ni kuisaidia timu ya taifa ya Uingereza na vipaji vya wachezaji wa Kiingereza kuweza kuwa na mafanikio ya kimataifa,jambo ambalo limekuwa ni tatizo kwa miaka mingi.