Cardiff yapanda daraja ligi kuu England

Kocha wa Cardiff akishangilia na mashabiki
Image caption Kocha wa Cardiff akishangilia na mashabiki

Cardiff City imekuwa timu ya kwanza kujihakikishia nafasi ya kupanda daraja la ligi kuu soka nchini England msimu ujao licha ya sare ya bila kufungana na Charlton Athletic katika mchezo wa usiku huu.

Pointi moja waliyoipata, iliwatosha kabisa kuwafanya wawe miongoni mwa timu 20 zitakazo pambana msimu ujao kusaka ubingwa wa kombe la ligi kuu nchini England,ligi yenye mashabiki wengi duniani.

Hii imekuwa mara ya kwanza kwa Cardiff kurejea kwenye ligi ya juu zaidi nchini Uingereza baada ya miaka 51 ya kupambana kwenye ligi ndogo toka waliposhuka daraja mwaka 1962.

Cardiff inakuwa timu ya pili kutoka nchi ya Wales ambayo ni sehemu ya Taifa la Uingereza kushiriki ligi kuu baada ya Swansea iliyopanda daraja misimu miwili iliyopita. Pia inakuwa timu ya 46 tofauti kushiriki ligi kuu nchini England toka ilipoitwa ligi kuu ya England mwaka 1992.

Misimu mitatu iliyopita,Cardiff ilijitahidi kupanda daraja lakini ilijikuta ikishindwa baada kutolewa kwenye michezo ya mtoano,lakini msimu huu umekuwa wa mafanikio kwa klabu hiyo ambayo inanolewa na kocha Malcolm George kutoka Scotland.

Image caption Mmiliki wa klabu ya Cardiff,Vincent Tan

Miaka mitatu iliyopita,wiki chache baada ya kufungwa na Blackpool na kupoteza nafasi ya kwenda ligi kuu,Cardiff ilijikuta kwenye matatizo makubwa baada ya kufikishwa mahakamani mara tatu baada ya kushindwa kulipa deni la malimbikizo ya kodi. Lakini deni hilo lilikuja kulipwa lote kwa pamoja na Bilionea Vincent Tan kupitia kampuni yake ya Malaysian Consortium ya Malaysia,ambayo iliwekeza kiasi cha paundi milioni 60 kwenye klabu hiyo.

Timu nyingine zitakazopanda daraja msimu ujao kwenye ligi ya Uingereza na zile zitakazoshuka kutoka ligi kuu kwenda ligi ya chini zitajulikana mwishoni mwa mwezi ujao.