Mbio za Arsenal zasimamishwa na Everton

Ligi kuu soka nchini England imeendelea tena usiku wa leo kwa mechi kati ya Arsenal The Gunners waliokuwa nyumbani kuwakaribisha Everton kwenye uwanja wa Emirates.

Kiungo wa Arsenal,Sant Cazorla akitoka uwanjani na masononeko
Image caption Kiungo wa Arsenal,Sant Cazorla akitoka uwanjani na masononeko

Mechi hiyo iliyowakutanisha makocha wawili waliodumu na timu zao kwa muda mrefu zaidi nyuma ya Sir.Alex Ferguson wa Manchester United,Ilimalizika kwa sare tasa ya bila kufungana.

Arsenal ambayo ipo katika harakati za kutafuta uwezekano wa kumaliza kwenye nafasi nne za juu za msimamo wa ligi kuu soka nchini England msimu huu,walijikuta wakiambulia pointi moja ambayo imewafanya kusalia kwenye nafasi ya tatu wakiwa na pointi 60 mbele ya Chelsea ambayo inakamata nafasi ya nne wakiwa na pointi 58 na michezo miwili ya ziada kwenye msimamo wa ligi.

Mechi hii imekuwa mechi ya nne kwa Arsenal kucheza mfululizo bila kufungwa kwenye ligi kuu,wakiwa wameshinda mara tatu na kutoka sare moja ambayo ni ya leo katika mechi nne zilizopita.

Safu ya ushambuliaji ya Arsenal ambayo imekuwa ikiongozwa na mfaransa Olivier Giroud kwa mara nyingine imeshindwa kuisadia klabu hiyo inayonolewa na kocha Arsene Wenger kupata magoli baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi katika mchezo huo.

Kwa matokeo ya leo,Everton wameendelea kusalia kwenye nafasi ya sita kwenye msimamo wakiwa na pointi 56 nyuma ya Tottenham Hotspur wenye point 58 wakiwa kwenye nafasi ya tano.

Mechi nyingine ya ligi kuu soka nchini England itapigwa jumatano ya tarehe 16 mwezi wa April kwenye Uwanja wa Upton Park kati ya wenyeji West Ham United watakaokuwa wakiwavaa vinara wa ligi hiyo Manchester United.

United,Inahitaji point nne tu ili iweze kujihakikisha ubingwa wa 20 wa ligi kuu msimu huu.

Mechi hiyo itachezwa majira ya saa nne kasorobo kwa saa za Afrika Mashariki.

Mechi nyingine zitakazochezwa jumatano usiku ni pamoja na Manchester City ambao watakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Etihad kuwakaribisha Wigan.Timu hizi mbili zitakutana tena baadaye tarehe 10 mwezi ujao kwenye fainali ya kombe la FA.

Mashariki mwa jiji la London kutakuwa na moja ya mchezo wa watani wa jadi kati ya Chelsea watakaokuwa wakipambana na Fulham kwenye uwanja wa Craven Cottage.Chelsea wanakutana na Fulham baada ya kutolewa kwenye kombe la FA na Manchester City wikiendi iliyopita,hivyo ushindi kwenye mchezo huu utaendelea kuwahakikishia uwezekano wa kushiriki michuano ya kombe la klabu bingwa msimu ujao.