Maandalizi ya London Marathon yakamilika

Image caption umati wa washiriki katika mbio zilizopita

Watayarishaji wa mbio za London Marathon wanasema matayarisho yamekwenda vyema licha ya kuimarishwa kwa usalama.

Matayrisho hayo yamejadiliwa sana kuliko kawaida kutokana na mashambulio ya mabomu katika marathon ya Boston mnamo siku ya Jumaatatu ya wiki iliyopita.

Polisi wameongezwa kwa takriban asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka jana ili kuwahakikishia usalama wakimbiaji na watazamaji.

Wakati huo huo mfuko wa hisani wa London Marathon utatoa pauni millioni £3.5 kwa zaidi ya miradi 90 ya michezo.

Zaidi ya wakimbiaji 35,000 wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo zimazoanza mtaa wa Blackheath kusini mashariki ya London na kumalizikia karibu na kasri ya Malkia ya Buckingham Palace.

Mshindi wa mwaka jana Wilson Kipsang na wakenya wenzake Patrick Makaou na Geoffrey Mutai wanakabiliwa na upinzani mkali wa Tsegaye Kebede na Ayele Abshero kutoka Ethiopia na bingwa wa Olympiki Stephen Kiprotich wa Uganda.

Kwa upande wa wanawake mchuano mkali unatazamiwa kati ya wakenya Priscah Jeptoo, Lucy Kabuu na Florence na Edna Kiplagat na bingwa wa Olympiki kutoka Ethiopia Tiki Gelana.