Di Canio azidi kuipaisha Sunderland.

Image caption Kocha wa Sunderland Di Canio akishangilia ushindi

Ligi kuu soka nchini England imeendelea wikiendi hii kwa michezo saba kufanyika jumamosi ya leo ambapo ilikuwa ni jumamosi ngumu kwa timu nyingi.

Hati hati ya kushuka daraja kwa timu tatu zinazoburuza mkia kwenye msimamo wa ligi ndo ilikuwa hadithi iliyotawala vichwa mbalimbali vya habari nchini Uingereza.

Lakini Sunderland baada ya kuwatandika watani zao wa jadi Newcastle wikiendi iliyopita kwa mabao 3-0,hii leo walikuwa nyumbani kwenye viunga vya Stadium of Light kuwakaribisha Everton.

Kwa mara nyingine, Kocha muitaliano Paulo Di Canio aliendelea kuwapa furaha mashabiki wa Sunderland baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi wa pili mfululizo dhidi ya Everton.

Stephane Sessegnon ndiye alikuwa shujaa wa leo,ambaye alifunga bao la pekee kwa Sunderland kwa shuti kali lililoshindwa kudakwa na Tim Howard mlinda mlango wa Everton,dakika chache kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.

Hii imekuwa mara ya kwanza kwa Sundeland kuifunga Everton tangu mwaka 2001 kwenye ligi kuu soka nchini England ambapo mara ya mwisho ilikuwa miaka 12 iliyopita katika msimu wa ligi ambayo Di Canio alikuwa mchezaji wa West Ham United. Msimu huo wa 2001,Di Canio alifanya kitendo ambacho kilimpa tuzo maalumu ya uchezaji wa kiungwana ama Fair Play Award baada ya kuudaka mpira akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga na kumuonyesha mwamuzi kuwa golikipa wa Everton Paul Gerrard alikuwa ameumia.

Matokeo haya yanaifanya Sunderland kupanda hadi nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 37,lakini kocha Di Canio anasema bado timu hiyo ipo kwenye wakati mgumu na anahitaji kuona anapata ushindi kwenye michezo yote iliyosalia.