Bayern yaitandika 4-0 Barcelona

Image caption Wachezaji wa Bayern Munich wakishangilia bao la kwanza

Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich wamejiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya baada ya kuitandika Barcelona 4-0 katika mchezo wa kwanzawa nusu fainali nchini Ujerumani.

Mabao mawili ya Thomas Müller, na yale ya Mario Gomez na Arjen Robben yaliizamisha Barcelona ambayo ilikuwa na nyota wake wote wakutegemewa,akiwemo Messi ambaye alikosa michezo kadhaa kabla ya kuanzishwa usiku huu.

Hii imekuwa mara ya kwanza kwa Barcelona kufungwa mabao 4-0 tangu mwaka 1997 walipofungwa na Dynamo Kiev ya Urusi mwaka 1997 kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani ulaya.

Bayern Munich wametoka kutawazwa kuwa mabingwa wa Ujerumani wiki chache zilizopita na iwapo watafanikiwa kuiondosha Barcelona na kutinga hatua ya fainali ya michuano ya klabu bingwa, itakuwa fainali yao ya tatu kushiriki ndani ya miaka minne.

Kocha wa Bayern Munich Jupp Heynckes awali alisema haogopeshwi na urejeo wa Lionel Messi,na katika mchezo huo Messi hakuonekana kuwa katika kiwango chake cha siku zote.

Matokeo haya yanafanya mchezo wa marudiano utakaochezwa wiki ijayo kuwa mgumu kwa Barcelona kwani haijawahi kutokea timu kwenye michuano ya klabu bingwa barani Ulaya kufungwa magoli manne na zaidi katika mchezo wa kwanza kisha kuyarejesha katika mchezo wa marudiano na kufuzu hatua inayofuata.

Baada ya Bayern Munich kuichabanga Barcelona, Jumatano usiku mahasimu wa Barcelona, Real Madrid nao watakuwa na kibarua kikubwa mbele ya Borussia Dortmund kwenye uwanja wa Signal-Iduna-Park,mchezo utakaofanyika majira ya saa nne kasorobo kwa saa Afrika Mashariki.