Mourinho kuihama Real Madrid msimu ujao

Jose Morinho
Image caption Jose Morinho kocha wa Read Madrid

Kocha wa Real Madrid Jose Mourinho, amesema huenda asiwe kocha wa klabu hiyo msimu ujao.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka hamsini, ambaye amewahi kuongoza Chelsea, siku ya Jumanne, alishuhudia vijana wake wakiondolewa kwenye nusu fainali ya michuano ya kuwania kombe la klabu bingwa barani Ulaya, licha ya kuilaza Borussia Dortmund ya Ujerumani, kwa magoli mawaili kwa yai.

Dortmund ilifuzu kwa fainali ya kombe hilo kwa jumla ya magoli manne kwa matatu.

Katika mechi ya raundi ya kwanza Dortmund, iliilaza Real Madrid kwa magoli manne kwa moja.

Kumekuwa ya ripoti kuwa kocha huyo kutoka Ureno, alikuwa akijiandaa kukihama klabu hiyo ya Real Madrid na kurejea nchini Uingereza.

Baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ya jana Morinho alisema , anafahamu kuwa anapendwa na mashabiki na vilabu vingi nchini Uingereza.

Hata hivyo amesema atasalia hadi mwisho wa msimu huu kabla ya kuamua hatma yake ya siku zijazo.

Mourinho alikihama klabu ya Chelsea, katika hali ambayo haikufahamika Septemba mwaka wa 2007, baada ya kutofautiana na mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich.