Messi na babake wadaiwa kulaghai serikali

Image caption Lionell Messi

Mshambulizi matata wa Barcelona Lionel Messi na babake wanachunguzwa nchini Uhispania kwa kuilaghai serikali ya nchi hiyo zaidi ya pauni milioni tatu nukta nne.

Mchezaji huyo kutoka Argentina na babake, Jorge wanatuhumiwa kuibia serikali ya nchi hiyo, kwa kujaza fomu zizizokuwa za ukweli za marejesho ya kodi kati ya mwaka wa 2007 na 2009.

Hata hivyo mechezaji huyo mwenye umri wa miaka ishirini na mitano hajasema lolote kuhusiana na madai hayo.

Messi hulipwa Euro milioni kumi na sita kila mwaka na ndiye mchezaji anayelipwa kiasi cha juu zaidi duniani.

Lakini mwendesha mashtaka Raquel Amado, aliwasilisha nyaraka za mahakama nyumbani kwake kwa mchezaji huyo katika mtaa wa kifahari wa Gava mjini Barcelona.

Jaji mjini humo ni sharti waidhinisha malalamishi dhidi ya mshukiwa yeyote kabla hajafunguliwa mashtaka.

Messi na babake wanashukiwa kutumia kampuni katika mataifa ya ngambo, mjini Belize na Uruguay kuuza haki za kutumia picha ya mchezaji huyo.

Mchezaji huyo na babake wanatuhumiwa kutumia kampuni hizo zilizoko nje ya Uhispania, ambako anaishi na kucheza soka ya kulipwa, kukwepa kulipa kodi inayokisiwa kuwa pauni milioni tatu na nusu.