NFF kuchagua wachezaji wa Super Eagles

Image caption Stephen Keshi

Rais wa shirikisho la mchezo wa soka nchini Nigeria, NFF Aminu Maigari ametangaza kuwa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo ya soka Stephen Keshi, hatakuwa tena na jukumu la kuchagua kikosi cha timu hiyo mwenyewe.

Maigari amehoji kikosi kilichoteuliwa kuakilisha Nigeria, katika fainali ya kombe la shirikisho inayoendelea nchini Brazil, ambayo Super Eagles iliondolewa katika raundi ya kwanza.

Rais huyo wa NFF amesema, hawajaridhika na matokeo ha timu hiyo.

''Kombe la shirikiso ni mashindano makubwa na ndio sababu mataifa mengine yaliteuwa vikosi ambavyo vina wachezaji wazuri zaidi'' Alisema Maigari.

Amehoji ni kwa nini Nigeria haikuteuwa wachezaji wake wazuri zaidi kama mataifa mengine kama vile Uhispania ambao watacheza kwenye fainali na Brazil.

Amesema mtindo huo haupaswi kuendelea alifoka kiongozi huyo wa NFF.

''Nigeria inawachezaji wengi ambao wana uzoefu na ujuzi na sielewi ni kwa nini waliachwa nje'' Aliongea Maigari.

Image caption Aminu Maigari

Hata hivyo matamshi hayo yameshutumiwa vikali na washika dau wa soka nchini humo miongoni mwao kocha Stephen Keshi.

Keshi amesema licha ya kuwa anafahamu ghadhabu za raia wa nchi hiyo kuhusu matokeo yao haifai kwa NFF kuingilia kati masuala ya timu hiyo ya taifa kwa kuwa hawana ujuzi na ufundi unaohitajika.

Mwezi Februari mwaka huu Keshi alitangaza kujiuzulu baada ya kuongoza Nigeria kushinda kombe la Mataifa bingwa barani Afrika nchini Afrika Kusini kwa mara ya kwanza Tangu mwaka wa 1994, kufuatia mzozo za NFF.