Kemboi anyakua medali ya dhahabu

Image caption Ezekiel Kemboi mwanariadha wa Kenya

Ezekiel Kemboi ameshinda ubingwa wake wa tatu wa dunia wa mbio za meta 3000 kuruka maji na viunzi katika mashindano ya ubingwa wa dunia wa riadha mjini Moscow.

Bingwa huyo mara mbili wa Olympiki mwenye umri wa mika 31 alikimbia mbio hizo kwa muda wa dakika 8 na sekunde 06.01 kunyakua medali ya dhahabu ,huku mkenya mwenzake Conseslus Kipruto mwenye umri wa 18 akishinda medali ya fedha kwa kukimbia mbio hizo kwa dakika 8 na sekunde 06.37 na Mahiedine Mekhissi Benabbad wa Ufaransa alipata medali ya shaba kwa dakika 8 na sekunde 07.86 na kuipokonya Kenya fursa ya kusomba medali zote kwa kumpiku Paul Kipsiele Koech.

Wakenya wanne katika fainali hiyo ndio waliyoongoza mbio hizo kuanzia mwanzo.

Benabbad alionekana kutishia kuwapita lakini Kemboi aliongeza kasi na kuthibitisha kua ni mwanariadha hodari kutoka Kenya katika miaka ya hivi karibuni.

Kemboi ameifikia rekodi ya Mkenya mwenzake Moses Kiptanui ya kushinda ubingwa wa dunia mara tatu mfululizo katika ya miaka 1991-1995.