Abramovich asitisha ufadhili wa soka Urussi

Image caption Roman Abramovich

Mfanya biashara tajiri na mmiliki wa klabu ya Chelsea, Roman Abramovich amesema amesitisha ufadhili wake wa soka nchini Urussi.

Msemaji wa kampuni ya uwekezaji ya Millhouse inayomilikiwa na Abramoviich, amesema, chuo cha mafunzo ya soka nchini Urussi kilichokuwa kikifadhiliwa na mfanyabiashara huyo kimeafikia malengo yake.

Mtandao wa Forbes umechapisha habari kuwa tangu mwaka wa 2010, Abramovich amekuwa akipunguza ufadhili wake kwa shughuli za kuimarisha soka nchini Urussi.

Hata hivyo hakuna mzozo wowote uliosababisha uamuzi huo.

Ripoti zinasema kampuni ya NFA ilifadhili ujenzi wa viwanja mia moja thelathini nchini Urussi na kutumia zaidi ya dola milioni mia mbili.

Kampuni hiyo iliyoundwa mwaka wa 2004, pia iligharamia mafunzo ya makocha nchini Urussi. Abramovich alianza kufadhili soka nchini Urussi muda mfupi baada ya kununua klabu ya Chelsea inayoshiriki ligi kuu ya Premier ya Uingereza.

Tangu mwaka wa 2005 hadi mwaka wa 2010 Abramovich alisaidi kufadhili timu ya taifa ya soka ya Urussi, ikiwa ni pamoja na mshahara wa dola milioni saba kwa kocha wake Guss Hiddink raia wa Uholanzi.

Dick Advocaat aliteuliwa kuwa kocha wa Urussi mwakam wa 2010 kuchukua mahala pa Hiddink.

Lakini mwaka wa 2010 Urussi ilishindwa kufuzu kwa fainali ya kombe la dunia iliyoandaliwa nchini Afrika Kusini.

Jarida la Forbes limechapisha ripoti kuwa Abramovich anashikilia nafasi ya kumi na tatu miongoni mwa watu tajiri zaidi nchini Urussi na inakadiriwa kuwa ana mali inayokisiwa kuwa zaidi ya dola bilioni kumi nukta mbili.