Kocha wa Nigeria Stephen Keshi matatani

Image caption Stephen Keshi

Shirikisho la mchezo wa soka duniani FIFA, limethibitisha kuwa limepokea malalamishi kutoka kwa shirikisho la mchezo wa soka nchini Malawi FAM, kuhusiana na matamshi yaliyotolewa na kocha wa Nigeria, Stephen Keshi.

Hata hivyo shirikisho hilo la FIFA limesema kuwa kwa sasa haliwezi kusema lolote kuhusu suala hilo, hadi uchunguzi utakapo kamilika.

FAM limedai kuwa Keshi alitoa matamshi ya ubaguzi dhidi ya kocha wake Tom Sainfiet raia wa Ubelgiji.

Katibu mkuu wa FAM, Suzgo Nyirenda ameiambia BBC, kuwa matamshi hayo ya ubaguzi hayafai kuwepo katika michezo katika dunia ya sasa.

''Tunahisi na shambulio dhidi ya kocha wetu na tutamtetea kwa hali na mali, bila kuzingatia uraia wake na rangi ya ngozi yake'' Alisema Nyirenda.

''Tumetuma ushahidi wa yale Keshi aliyoyasema na tunatarajia kuwa FIFA itachukua hatua kali dhidi ya kocha huyo wa Nigeria Stephen Keshi'' aliongeza Nyirenda.

Kesi hiyo inahusiana na matamshi ambayo Keshi aliyatoa kufuatua wito wa Malawi wa kuhamisha mechi yao ya kufuzu kwa kombe la dunia mwaka wa 2014, kutoka mji wa Calabar kutokana na sababu za kiusalama.

Katika mahojiano na runinga moja ya Uingereza, Keshi alisema ''Nafikiria kuwa kocha huyo wa Malawi ni wazimu''.

''Ikiwa anataka kuongea na FIFA, basi ni lazima arejea kwao nchini Ubelgiji. Yeye sio mtu wa Afrika, ni mzungu mweupe, ni lazima arudi kwao Ubelgiji'' Alisema Keshi katika mahojiano hayo.

Maafisa wakuu wa shirikisho la mchezo wa soka nchini Nigeria pamoja na kocha huyo hawajasema lolote kuhusiana na madai hayo ya kocha wa Malawi Saintfiet na FAM.

Mechi hiyo kati ya Malawi na Nigeria mjini Calabar itaamua nani atafuzu kwa raundi ya mwisho ya mechi ya kufuzu kwa fainali hiyo barani Afrika.

Mabingwa hao wa Afrika wanahitaji kutoka sare ya aina yoyote ili kufuzu ili hali Malawi inahitaji ushindi ili isonge mbele.