Arsenal 2 Fenerbahce 0

Image caption Nyota wa 'The Gunners' uwanjani

Aaron Ramsey alifunga mabao mawili na kuipa klabu yake Arsenal ushindi wa wazi bila upinzani mkali dhidi ya Fenerbahce ya Uturuki.

Katika mechi iliyochezwa hapo jana kwenye uwanja wa Emirates, Arsenal imefuzu kwa Ligi ya Mabingwa kwa mwaka wa kumi na sita mfululizo.

Wageni Fenerbahce walibaki nyuma tangu mechi ya awamu ya kwanza walipofungwa mabao matatu kwa bila na Arsenal. Adhabu hiyo kwa Fenerbahce imerahisisha kazi ya shirika la kandanda la Uropa, UEFA, kwani sasa haitajishughulisha kuizuia klabu hiyo kutoshiriki mechi ya ligi za mabingwa, hii inafuatia marufuku ya miaka miwili ambayo inafaa kutolewa kwa Fenerbahce baada ya kushtumiwa na hatia ya kupanga mechi.

Ikiwa klabu hiyo ingefaulu kushiriki Ligi ya Mabingwa basi kingekuwa kibarua kigumu kwa UEFA kutekeleza sheria na adhabu ipasavyo.

Hii leo jumatano, mahakama ya rufaa itasikiliza kesi hiyo.

Arsenal imewahi kushindwa na timu za Uropa mara mbili tu katika muda wa miaka hamsini, huku klabu hiyo ya Uturuki imepata kufunga mabao mara tatu tu katika ziara zake nane za England.