Mourinho apuuza ushindi wa Bayern

Bayern Munich dhidi ya Chelsea
Image caption Bayern Munich dhidi ya Chelsea

Jose Mourinho alidai baada ya mechi kua timu bora ndiyo iliyopoteza kufuatia ushindi wa Bayern Munich dhidi ya watu 10 wa Chelsea kwa matuta 5-4 kufuatia suluhu ya bao 2-2 katika mchuano wa kombe la Uefa la Super Cup.

Chelsea ilionekana kukaribia ushindi zikiwa zimesalia sekunde chache kipenga cha kumaliza mechi kipigwe mjini Prague, lakini mchezaji aliyeingizwa katika mda wa majeruhi Javi Martinez akarudisha na kusababisha mda wa ziada na hivyo kusababisha mshindi aamuliwe kwa njia ya matuta.

Mchezaji Romelu Lukaku ndiye aliyekosa mkwaju wa mwisho ambao ungeamua mshindi lakini Mourinho hata hivyo kama kawaida alionekana kua katika hali ya ubabe bila kutaka kukubali matokeo.

"timu bora wazi wazi imepoteza," alisema. "wametushinda kwa sababu ya kufunga mkwaju mmoja zaidi yetu."

Awali mshambuliaji Fernando Torres aliipa Chelsea bao la kwanza katika kipindi cha kwanza lakini Franck Ribery akarudisha dakika mbili baada ya kipindi cha pili kuanza na kupelekea mchezo uingia mda wa ziada.

Mnamo dakika ya 85 mcheza kiungo Ramires akaonyeshwa kadi nyekundu na kuwaacha washindi wa Ligi ya Europa League uchi. Ingawa Eden Hazard aliirejeshea Chelsea matumaini katika kipindi hiki cha ziada, Martinez aliusukuma mpira wavuni sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho kusababisha mechi kuamuliwa kupitia matuta.