Atsu aridhia hatua ya Chelsea

Image caption Christian Atsu

Mchezaji soka Christian Atsu raia wa Ghana ameelezea furaha yake kwa kusajiliwa na kilabu ya Chelsea katika kipindi kilichokamilika cha uhamisho wa wachezaji.

Mustakabali wa mchezaji huyo wa kiungo cha kati kwenye timu ya Ghana, ilikuwa haijulikani pakiwa na ati ati kuhusu ambako angesajiliwa.

Lakini alitia saini mkataba wa miaka mitano na Chelsea ingawa kilabu hiyo imemtoa kwa mkopo kwa kilabu ya Vitesse.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, anaweza kucheza kama mshambulizi.

Atsu amekuwa vinywani mwa watu sana nchini Ghana wakati huu na wengi hawajafurahia sana kuhusu hatua hii yake.

Atsu amerejea Ghana akijiandaa kwa mchuano wa kufuzu kushiriki kombe la dunia dhidi ya Zambia mjini Kumasi.

Kuna hisia kali miongoni mwa wachezaji na mashabiki pamoja na wadadisi wa soka kuwa mktaba huo haitaimarisha mchezo wa Atsu.

Hata hivyo Atsu amesema amefurahishwa sana na hatua ambayo Chelsea imeichukua akisema kuwa kama mchezaji ni muhimu kucheza ili kusalia katika hali nzuri.

Amesema atajitahidi kufanikisha mpango huu ili aweze kuwekwa na mkufunzi wa kilabu hiyo Jose Mourinho kwenye mipango yake ya siku za baadaye Chelsea.

"wakati Chelsea iliponichukua , niliona nafasi nzuri kufanya kazi na kilabu kubwa na kocha mzuri. ''

"najua lazima nionyeshe mchezo wangu nikichezea Vitesse mwanzo na nitafanya vivo hivyo.''

Alisema kuwa kuwepo kwa Michael Essien Chelsea , ndiko kulichochea uamuzi wake kwenda Stamford Bridge.