Mwanariadha wa Kenya Kemboi kustaafu

Image caption Ezekiel Kemboi kwenye mashindano ya Moscow

Mwanariadha wa kenya mwenye mbwembwe Ezekiel Kemboi ametangaza mpango wake wa kustaafu baada ya michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 2016 mjini Rio de Janeiro huko Brazil .

Kemboi anayesifika kwa mbio za kuruka maji na viunzi analenga kushinda medali ya Dhahabu kwa mara ya tatu katika mbio za Olimpiki.

"Nimeiwakilisha Kenya kwa muda wa miaka 13 mtawalia, nitakamilisha maisha yangu kama mkimbiaji baada ya Rio 2016" Kemboi alidokeza katika hafla ya zawadi mjini Eldoret eneo la Bonde la ufa.

Mwanariadha huyo mshindi mara mbili wa Olimpiki na mara tatu duniani atajitosa katika mchezo wa Golf atakapostaafu. Mchezo huo utajumuishwa kama mchezo wa Olimpiki mwaka 2016.

Kemboi mwenye umri wa miaka 31 alimshinda Conseslus Kipruto ili kupata taji lake la tatu la mkimbiaji bora duniani wa kuruka maji na viunzi kwa wanaume mjini Moscow mwezi uliopita