Wachezaji walichongea kufutwa Di Canio

Image caption Kocha Di Canio

Inaarifiwa wachezaji wa Sunderland walilalamika kwa mkurugenzi mkuu wa klabu hiyo Margaret Byrne kuhusu kocha Paolo Di Canio kabla ya kupigwa kalamu.

Di Canio aliitisha mkutano wa timu nzima siku ya Jumapili ambao inasemekana ulikumbwa na majibizano makali kufuatia timu hiyo kushindwa mabao 3-0 na West Bromwich Albion.

Baadae wachezaji waandamizi walimwambia Byrne kwamba hali imekua isioweza kuvumilika kwa sababu ya tuhuma kali na matusi ya Mtaliana huyo dhidi ya kikosi cha timu hiyo.

Kikosi hicho ambacho hujulikana kama 'The Black Cats' wameambua pointi moja tu kutoka mechi tano za ligi ya Premier League katika msimu huu.

Aliyekua kocha wa Chelsea na West Brom Roberto Di Matteo ndie anaetabiriwa na wengi kuteuliwa kuwa kocha mpya na wengine wanaotajwa ni Gus Poyet, Tony Pulis na Alex McLeish.

Kocha msaidizi Kevin Ball ameteuliwa kua kaimu kocha kwa hivi sasa.

Di Canio ameshinda mechi 3 tu kati ya 13 baada ya kupigwa kalamu Martin O'Neill mnamo mwezi wa Machi.