Bayern Munich waiadhibu Man City

Image caption Kocha wa Bayern Pep Guardiola

Bayern Munich imeonyesha nia ya kutetea ubingwa wa vilabu Ulaya kwa kuicharaza Manchester City ya England kwa mabao matatu kwa moja. Katika pambano liliotia fora kati ya michuano ya Jumaatano ya kuwania kombe la klabu bingwa ya Ulaya.

Mlinda lango wa City Joe Hart amelaumiwa kwa kuchangia katika mabao ya Bayern. Kwanza akikosa kuokoa mkwaju kutoka masafa ya mbali wa Franck Ribery na pia kufungwa kwa urahisi na Arjen Robben bao la tatu liliothibitisha ushindi uliostahili kwa kikosi cha Pep Guardiola.

Thomas Muller alifunga bao la pili la Bayern.Mchezaji wa akiba Alvaro Negredo aliipatia City bao la kufuta machozi la City.

Beki wa zamani wa City Jerome Boateng alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumpiga mueleka Yaya Toure wakati City ikiimarisha mashambulizi ambayo hayakufua dafu.

Majirani wa City ambao pia ni watani wao wa jadi , Manchester United walitoka sare1-1 na Shakhtar Donetsk ya Ukraine baada ya kufungua mlango lakini Tyson akaondoa matumaini ya ushindi ya United kwa kufunga bao zuri la kusawazisha.

Huko Hispania,Real Madrid waliicraza F.Copenhagen ya Denmark 4-0 na Paris Saint Germain ya Ufaransa nayo ikaizaba Benfica ya Ureno 3-0 na Juventus ya Italia ikatoka sare ya 2-2 na Galatasary ya Uturuki.