Everton yapoteza mara ya kwanza

Yaya Toure
Image caption Yaya Toure

Manchester City imeondoa rekodi ya mwanzo mzuri wa Everton kutopoteza mechi hata moja tangu kuanza kwa msimu huu wa 2013/14.

Ushindi huu kwa Man City ni habari nzuri kwa mashabiki wa City iliyochapwa katikati ya wiki na bingwa mtetezi wa Ligi ya mabingwa barani Ulaya Bayern Munich ya Ujerumani.

Everton iliongoza kwa bao la Romelu Lukaku lililopenyezwa kwapani mwa golikipa Joe Hart anayepitia kipindi kigumu.

Bao hilo lilifutwa na la Alvaro Negredo baada ya kupokea pasi kutoka kwa kiungo Yaya Toure.

Baada ya mda mkwaju wa chini chini wa mshambuliaji Sergio Aguero ukaipa City uongozi wa magoli 2-1 kabla ya mkwaju wake wa peneti uliogonga kichwa cha golikipa Tim Howard na kuishia kimyani.

Adhabu ya mkwaju huo ilifuatia kitendo cha Seamus Coleman kumkaba Pablo Zabaleta ingawa Everton walilalamikia uwamuzi huu wa bao ambalo baadaye uliandikishwa kama bao la kujifunga wenyewe.

Licha ya ushindi huu wa 3-1 kwa city na kushamiri katika mashambulizi bado kitengo chao cha ulinzi kinatia mashaka.

Vincent Kompany alionyesha kua kiongozi mzuri kati ya mabeki wanne walioshiriki mchuano wa Bayern lakini baada ya dakika 33 aliondolewa kwa kile kilichoonekana kama kuuguza misuli ya mguu.