Yaya Toure alalamikia ubaguzi viwanjani

Image caption ubaguzi umekuwa ukiwanyima raha wachezaji weusi

Kiungo wa kati wa Manchester City Yaya Toure ameonesha kughadhabishwa na kulitaka shirikisho la kandanda barani ulaya, UEFA kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ushangiliaji wenye kuashiria ubaguzi wa rangi, baada ya kudai kuwa vilifanyika dhidi yake timu yao ilipotoka na ushindi wa 2-1 jijini Moscow

Mchezaji huyo wa kimataifa kutoka Ivory coast alisema alimlalamikia mwamuzi wa mchezo huo Ovidiu Hategan kuhusu kitendo hicho, alipokuwa nahodha wa timu yake.

Toure anafikiri kuwa pengine shirikisho la soka barani ulaya litachukua hatua ya kufungia uwanja kwa miezi au miaka kadhaa.

Mwezi May, UEFA ilitangaza kuchukua hatua kwa vitendo vinavyoashiria ubaguzi wa rangi kwa kufungia kwa muda mfupi viwanja iwapo ni kosa la kwanza, na kufunga moja kwa moja kwa kosa la pili sambamba na adhabu ya kulipa pauni 42,800.