Wenger aonya kususia kombe la dunia

Yaya Toure

Siku moja baada ya Mchezaji wa kimataifa za soka wa Ivory Coast Yaya Toure,kulalamikia kuhusu shutuma za kufanyiwa vitendo vya ubaguzi wa rangi nchini Russia,Kocha wa Klabu ya Arsenal Arsene Wenger amesema ni mapema mno kutishia kususia Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 zitakazofanyika nchini Russia.

Kiungo huyo wa Manchester City Yaya Toure amependekeza kuwa Wachezaji wenye asili ya Afrika wanapaswa kuchukua hatua,baada ya kulalamikia vitendo vya ubaguzi hapo juzi wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya CSKA Moscow.

Kocha huyo wa Arsenal amesema Tunapaswa kupambana na vitendo vya ubaguzi nchini Russia na pengine popote pale,Lakini akaongeza kuwa Kufikiria kususia Fainali za kombe la Dunia mwaka 2018 ni hatua ya mbali zaidi kwa sasa.

Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limesema linafanya uchunguzi kuhusu madai hayo ya Yaya Toure,ingawa Russia tayari imekanusha kuwa hakukufanyika vitendo vyovyote vya ubaguzi wa rangi.