Tanzania na Zimbabwe zatoka sare

Image caption Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars

Timu ya soka ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars imetoka sare ya 0 - 0 na timu ya taifa ya Zimbabwe katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa mjini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Tanzania ilishindwa kutumia nafasi kadhaa ilizopata na hasa katika kipindi cha kwanza ambacho walicheza vizuri.

Ikiwatumia wachezaji wake nyota wanne wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi hiyo Tanzania iliwabana wageni wao ambao walicheza kwa kiwango kizuri kwenye kipindi cha pili.

Mechi hiyo ambayo imechezwa katika tarehe ya michezo ya kirafiki ya kimataifa ya FIFA imechezeshwa na waamuzi kutoka Uganda.

Awali Tanzania ilikuwa icheze na timu ya taifa ya Kenya kabla ya Kenya kujiondoa katika mchezo huo kutoka na matatizo ya maandalizi ya timu yao.

Kwa upande wake Zimbabwe ambao walipanga kucheza na Afrika Kusini nao hawakuweza kucheza nao baada ya kuambiwa Afrika ya Kusini imesitisha kucheza na nchi hiyo na badala yake watacheza mabingwa wa kombe la dunia timu ya taifa ya Hispania.

Mbali na kujipima nguvu Tanzania imetumia mchezo huo wa kirafiki kujiandaa na mashindano ya kombe la CECAFA kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu nchini Kenya.