CECAFA:Tanzania na Kenya nusu fainali

Image caption Timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars

Timu ya taifa ya Tanzania bara "Kilimanjaro Stars" imesonga mbele hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA Senior Challenge baada ya kuisambatisha timu ya Taifa ya Uganda, "Uganda Cranes" jumla ya mabao 5-4.

Timu hizo zilipambana katika uwanja wa Manispaa mjini Mombasa, Kenya, ukiwa ni mchezo wa kwanza kwa timu zilizotinga hatua ya robo fainali.

Uganda ndio waliokuwa wa kwanza kujipatia bao katika dakika ya 16 likifungwa na mshambuliaji wake Daniel Ssrenkuma.

Mrisho Ngassa aliisawazishia timu ya yake ya Kilimanjaro Stars dakika mbili tu baadaye akipokea pasi ya kisigino kutoka kwa Mbwana Samatta.

Ngassa huyo alishindilia goli la pili katika dakika ya 38 ya kipindi cha kwanza.

Hadi mapumziko Tanzania ilikuwa mbele kwa magoli 2-1. Kipindi cha pili timu hizo ziliendelea kushambuliana, huku Tanzania ikimpoteza mchezaji wake kiungo Salum Abubakar baada ya kupatiwa kadi nyekundu katika dakika ya 52 ya mchezo.

Mwanya huo uliwanufaisha Uganda na kuweza kusawazisha goli la pili katika dakika ya 75.

Image caption Timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars

Hadi dakika 90, timu hizo zilitoka sare ya kufungana magoli 2-2. Ndipo mikwaju ya penalti ilipotumika kumpata mshindi wa mechi hiyo.

Tanzania iliweza kutumbukiza penalti 3, huku Uganda ikiambulia 2. Mlinda mlango wa Kilimanjaro Stars, Ivo Mapunda alikuwa shujaa kwa kupangua mikwaju miwili kati ya mitatu iliyokosa lango.

Nayo Harambee Stars ya Kenya iliirarua Rwanda, Amavubi kwa goli 1-0.

Huo ulikuwa ni mchezo wa pili wa robo fainali ambao ulichezwa katika uwanja huo huo wa Manispaa mjini Mombasa.

Kwa matokeo hayo Kilimanjaro Stars itaonyeshana kazi na Harambee Stars katika mpambano wa nusu fainali utakaopigwa katika uwanja wa Kisumu, magharibi mwa Kenya.