3 wakamatwa kwa kupanga mechi Uingereza

Image caption Sam Sodje alikuwa mchezaji wa timu ya kitaifa ya Nigeria

Watu watatu wanazuiliwa na polisi nchini Uingereza baada ya aliyekuwa mchezaji wa Portsmouth kumwambia mwandishi wa habari kuwa alihusika katika kupanga mechi.

Sam Sodje alirekodiwa kwenye kanda ya video na mwandishi wa habari mmoja wa jarida la Sun akizungumzia alivyompiga mchezaji wa timu hasimu usoni katika ligi ya daraja la kwanza, ili apate kadi nyekundu na kisha baadaye alipwe pauni 70,000.

Alisema pia alipangia mchezaji mwingine aweze kulipwa pauni 30,000 kwa kupokea kadi ya manjano katika mechi ya ligi.

Klabu ya Portsmouth imeelezea kushtushwa sana na madai hayo.

Katika Kanda hiyo liyorekodiwa kisiri, bwana Sodje raia wa Nigeria, pia alidai ana uwezo wa kupanga mechi za ligi kuu na kuwa yuko tayari kupanga mechi katika kombe la dunia mwaka ujao.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, msemaji wa klabu hiyo, alisema kuwa ikiwa madai haya ni ya kweli, basi ijulikane kuwa ni ya kushtua na kushangaza sana , jambo la kupanga mechi bila shaka linaathiri pakubwa maadili ya mchezo wa soka.

Sodje hachezei tena klabu ya Portsmouth lakini itambidi ashirikiane na maafisa wakuu kwa uchunguzi.

Sodje aliondolewa uwanjani katika dakika ya 50 wakati wa mchuano kati ya Portsmouth na Oldham Athletic kwenye ligi ya daraja la kwanza tarehe 23 Februari mwaka 2013.