West Ham yaiadhibu Spurs

Image caption West Ham wakipambana na Tottenham

Mabao mawili katika dakika 10 za mwisho yaliipa ushindi West Ham dhidi ya Tottenham na kuiwezesha kuingia nusu fainali ya kombe la Capital One ambapo itapambana na Manchester City.

Tottenham walifungua mlango katika nusu ya pili wakati Emmanuel Adebayor alipofunga bao lake la kwanza tangu mwezi wa Mei.

Westham walisawazisha kupitia kwa Matt Jarvis na zikiwa zimesalia dakika tano mchezo huo kumalizika, Modibo Maiga alifunga kwa kichwa kutokana na krosi ya Mohamed Diame.

Mechi hiyo ilianza tu kusisimua katika dakika ya 67 pale Adebayor, ambaye hadi wakati huo alikuwa amecheza kwa jumla ya dakika 45 tu msimu mzima alipofunga bao. Lakini hatimaye Spurs walitoka wakiwa wamepigwa na butwaa kutokana na kipigo cha pili mfululizo nyumbani kwao wiki hii baada ya kuchapwa 5-0 na Liverpool, siku ya Jumaapili na kusababisha kocha Andre-Villas Boas kupigwa kalamu.

Katika mchuano mwinginge klabu bingwa ya ligi ya England Manchester United nao pia walipiga hatua ya kuingia nusu fainali ya kombe hilo kwa kuicharaza Stoke City mabao 2-0 yaliyofungwa na Ashley Young na Patrice Evra katika mchezo uliosimamishwa kwa muda kutokana na mvua. Katika nusu fainali United wamewaepuka majirani na watani wao wa jadi Manchester City,na watapambana na Sunderland waliowatoa Chelsea siku ya Jumaanne.