Arsenal yapoteza uongozi wa ligi

Image caption Mchezaji wa Arsenal akikabiliana na mchezaji wa Chelsea

Harakati za Arsenal za kurejea tena kileleni mwa ligi kuu ya Premier ya England ziliambulia patupu pale ilipotoka sare ya tasa na Chelsea, katika uwanja wao wa nyumbani wa Emirates.

Kufuatia tasa hiyo, Liverpool imetwaa nafasi ya kwanza msimu huu wa Krismasi, huku Arsenal ikiwa ya pili na alama sawa lakini inadunishwa na idadi ya magoli.

Frank Lampard nusura aiifungie Chelsea wakati mkwaju wake ulipogonga paa la goli katika kipindi cha kwanza, naye Olivier Giroud alipoteza nafasi mbili nzuri za kufunga.

Refa wa mechi hiyo Mike Dean, alikemewa na mashabiki wa Arsenal ambao walihisi kuwa refa huyo alikuwa akiegemea upande wa Chelsea kutokana na maamuzi yake.

Wakati wa mechi hiyo, refa huyo alichukua maamuzi ambayo wengi bado wangali wanayazungumzia.

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger anasema walistahili kupewa penalti pale mlinda lango wa Chelsea Willian alipomuangusha Theo Walcott ndani ya kijisanduku.

John Mikel Obi vile vile aliepuka kadi nyekundu katika kipindi cha kwanza pale alipomfanyia madhambi Mikel Arteta kitendo ambacho kilimuepuka refa wa mechi hiyo.

Hatua chache kutoka uwanja huo wa Emirates, Klabu ya Tottenham imemteua Tim Sherwood kuchukua mahala pa Andre Villas-Boas kama kocha wa klabu hiyo.