Arsenal watesa ligi kuu England

Image caption Washambuliaji wa Arsenal, Olivier Giroud na Theo Walcot

Kinyang'anyiro cha ubingwa wa ligi kuu ya England kimezidi kupamba moto, ambapo miamba wa ligi hiyo timu za Arsenal, Manchester City, Chelsea na Everton, wakiwa katika nafasi nne za kwanza baada ya timu zote 20 za ligi hiyo kucheza mechi 19.

Arsenal bado ni vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 42, wakifuatiwa kwa karibu na Manchester City yenye pointi 41, huku Chelsea ikijikusanyia jumla ya pointi 40 na Everton wakitia kibindoni pointi 37.

Kabla ya mchezo huo wa 19, Manchester City ndio iliyokuwa ikiongoza ligi hiyo, huku Liverpool ambayo kwa sasa ipo katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 36 iliwahi kukalia kiti hicho wakati wa Krismasi. Manchester United imejikongoja na sasa inashika nafasi ya sita kwa kuwa na pointi 34.

Kivumbi kingine ni katika kuepuka kushuka daraja, ambapo Crystal Palace ambayo kwa muda mrefu ilikuwa katika hatari ya timu tatu zinazoshuka daraja, imejivuta hadi nafasi ya 17 ikiwa na pointi 16.

Timu za Fulham, West Ham na Sunderland ndizo zilizo katika ukanda wa hatari zaidi wakati huu wa kuelekea mzungo wa pili wa ligi kuu ya England mwakani.