United yanyolewa nyumbani na Tottenham

Image caption Wachezaji wa Tottenham

Tottenham imeandiksiha ushindi wake wa pili mfululizi katika uwanja wa Old Trafford dhidi ya wenyeji Manchester United na kujizolea alama tatu muhimu na kupanda hadi nafasi ya sita kwenye msururu wa ligi kuu ya Premier.

Mabingwa hao watetezi, walianza vyema lakini Emmanuel Adebayor, alijikakamua na kuifungia Tottenham bao lake la kwanza kwa kichwa baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Christian Eriksen.

Eriksen naye akaongeza la pili baada ya kuchapa mkwaju mkali uliomuacha kipa wa Manchester United kinywa wazi.

Lakini katika kipindi cha pili Danny Welbeck akafufua matumaini ya United kwa kuifungia United bao moja na kufanya mambo kuwa Tottenham mawili United Moja.

Baada ya bao hilo la Welbeck United ilifanya mashambulio kadhaa katika lango la Tottenham lakini juhudi zao ziligongwa mwamba.

Image caption Wachezaji wa Man United baada ya kushindwa na Tottenham

Javier Hernandez nusura asawazishe dakika za mwisho mwisho lakini mkwaju wake ukaokolewa.

Matokeo hayo yalikuwa mazuri kwa kocha mpya wa Tottenham Tim Sherwood, ambaye hajashindwa katika mechi nne alizosimamia.

Kabla ya ushindi wao wa magoli matatu kwa mawili katika uwanja huo mwaka uliopita, Tottenham ilikuwa haijawahi kuishinda United katika uwanja wa Old Trafford kwa zaidi ya miaka 23.

Manchester United sasa inashikilia nafasi ya saba alama kumi na moja nyuma ya vinara wa ligi hiyo kwa sasa Arsenal iliyo na alama 45.

Manchester City ni ya pili alama moja nyuma ya Arsenal huku Chelsea ikiwa ya tatu na alama 43.