ManU wasiwasi kutetea ubingwa

Image caption David Moyes, meneja wa Manchester United

Kocha Mkuu wa Klabu ya Manchester United ya England, David Moyes amesema angependa kusajili baadhi ya wachezaji kuimarisha kikosi chake lakini ana wasi wasi huenda asiweze kuwapata wachezaji hao katika usajili wa dirisha dogo mwezi huu wa Januari.

Kiungo Marouane Fellaini ndiye mchezaji pekee aliyesajiliwa tangu kuwasili kwa David Moyes katika kikosi cha Manchester United kinachoshikilia nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kuu ya Kandanda ya England inayoendelea.

Kocha huyo amenukuliwa akisema kuwa "Tungependa kuongeza wachezaji lakini swali la kujiuliza,ni Je wanaweza kupatikana wachezaji hao"?

Akizungumza Jumapili baada ya kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Swansea kwenye kombe la FA, Kocha huyo amekiri kuwa kuna mahitaji makubwa ya wachezaji wapya ndani ya kikosi cha Manchester United, lakini hakuna umuhimu wa kutangaza jambo hilo kwa sababu wachezaji ambao angependa kuwasajili hawawezi kupatikana katika usajili wa dirisha dogo mwezi Januari.

Kocha huyo amekiri kuwepo kwa hali ya wasi wasi klabuni hapo msimu huu baada ya timu ya Manchester United kupoteza mechi nne kati ya sita zilizochezwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Old Traford.

Kichapo cha Jumapili cha mabao 2-1 dhidi Swansea kilikuwa cha pili katika kipindi cha miaka thelathini kwa Manchester United kuondolewa katika raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la FA, huku mwanasoka Wilfried Bonny akitia kambani bao la ushindi katika dakika ya 90, ushindi ambao ulikuwa wa kwanza kwa Swansea katika uwanja wa Old Traford,baada ya Javier Hernandes kusawazisha bao la kuongoza la Swansea lililotiwa kimiani mapema na Wayne Routledge.

Kipigo cha Jumapili dhidi ya Swansea ambacho ni cha saba katika michuano yote kwa ujumla msimu huu kimekuja kikifuatia kingine ambacho Manchester United ilikipata siku ya mwaka mpya baada ya kupigwa na Tottenham Hostspurs mabao 2-1.

Akizungumzia kipigo hicho kiungo Darren Fletcher amesema kuwa wachezaji wa Manchester waliwaangusha mashabiki na kocha wao huku akielezea kuwa hali hiyo imeleta maumivu na hasira kubwa kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo kufuatia mwenendo wa timu nzima msimu huu ambapo imepoteza mechi nne kati ya sita zilizochezwa katika uwanja wa nyumbani wa Old Traford.