Simpson amlalamikia mkufunzi wake

Image caption Sherone Simpson mwanariadha kutoka Jamaica

Mwanariadha wa michuano ya Olimpiki wa Jamaica Sherone Simpson ameliambia jopo la nidhamu la nchi hiyo, Jumanne kwamba si mtumiaji wa dawa za kuongeza nguvu mwilini wakati wa michezo na kamwe hajawahi kudhamiria kutumia dawa ambazo zimepigwa marufuku michezoni.

Mshindi huyo wa medali ya Fedha katika mbio za mita 400 katika michezo ya Olimpiki iliyofanyika London amelalamikia dawa alizopewa na mkufunzi wake Christopher Xuereb, kuwa ni sababu ya yeye kuonekana kuwa anatumia dawa za kusisimua misuli baada ya kuchukuliwa vipimo.

Simpson, mwenye umri wa miaka 29: "Hakuna nilichosoma kinachoonyesha kuwepo kwa tukio baya."

Alikuwa mmoja wa wanariadha watano wa Jamaica waliochukuliwa vipimo na kuonyesha wanatumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni katika ubingwa wa taifa mjini Kingston mwezi Juni mwaka 2013.

Image caption Asafa Powell mwanariadha wa Jamaica

Simpson na mwanariadha mwenzake, ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 100 Asafa Powell, walibainika kutumia dawa ya oxilofrine, inayosisimua misuli.

Sherone Simpson ni nani?

•Mwanariadha wa Jamaica. Alizaliwa Agosti 1984 •Alishinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 400 kupokezana vijiti katika michezo ya Olimpiki ya Athens ya mwaka 2004 •Mshindi wa medali ya fedha katika mita 100 katika michuano ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008 na mshindi pia wa medali ya fedha katika mbio za mita 400 katika michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012. •Vipimo alivyofanyiwa vilionyesha ametumia dawa ya oxilofrine iliyopigwa marufuku michezoni wakati wa mashindano ya kitaifa ya riadha nchini Jamaica mwezi Juni 2013. •Mkimbiaji mwenzake Asafa Powell naye alibainika kutumia dawa hizo wakati wa mashindano hayo.

Warusha kisahani Allison Randall na Travis Smikle, pamoja na mwanariadha mchanga, pia walibainika kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni katika mashindano hayo.

Simpson amedai kuwa moja kati ya aina sita ya virutubisho alivyopewa na mkufunzi wake Xuereb kimehusika katika matokeo hayo ya kusikitisha kwake na amesema ametafiti na kugundua kuwa kirutubisho aina ya "Epiphany D1'' ndicho kilichotoa matokeo hayo.

Hata hivyo Xuereb amekana kuwapatia Simpson na Powell aina yoyote ya virutubisho vilivyopigwa marufuku isipokuwa alinunua virutubisho vya vitamin vinavyoruhusiwa.

Amedai kuwa wanariadha hao wawili wanatafuta mtu wa kumtwisha mzigo wa tatizo lao.