Man City yailamba Rovers FA 5 - 0

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sergio Aguero

Mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero, alipachika bao dakika moja baada ya kurejea uwanjani, ambapo timu yake iliisambaratisha Blackburn Rovers kwa jumla ya mabao 5 - 0 na kujipatia nafasi ya kutinga mzunguko wa nne itakapochuana na Watford.

Mshambuliaji huyo wa Argentina amekuwa nje ya dimba kutokana na maumivu ya mguu, lakini alingia kipindi cha pili na kuwaasha moto wa magoli.

Hadi anaingia Manchester City walikuwa tayari wakiongoza kwa mabao matatu kwa bila baada ya Alvaro Negredo kupachika mabao mawili huku Edin Dzeko akipachika bao moja.

Baada ya Aguero kupachika bao wavuni, Dzeko aliunganisha vizuri krosi ya Jesus Navas na kufunga bao lake la pili.

Ulikuwa ni ushindi mwingine mnono wa vijana wa Manuel Pellegrini, ambao walitoka sare ya bao moja kwa moja katika mchezo wa awali uliopigwa katika dimba la Ewood Park. Timu hiyo sasa imefunga jumla ya magoli 99 katika mashindano yote msimu huu.