Afueni kwa wafanyikazi wa Qatar 2022

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kiwanja Qatar 2022

Kamati andalizi ya kombe la dunia mwaka wa 2022 itakayoandaliwa huko Qatar imetoa mustakabali mpya utakaosimamia uhusiano baina ya wenye kandarasi na wafanyikazi wa kigeni wanaojenga viwanja vitakavyotumika katika michezo hiyo.

Takriban wajenzi 200 raiya wa Nepal waliripotiwa kufariki katika miradi ya ujenzi mwaka uliopita.

Kulingana na Shirika la International Trade Union iwapo hali itasalia ilivyo sasa nchini Qatar wafanyi kazi takriban 4000 watakuwa wamepoteza maisha yao katika ujenzi wa viwanja na muundo msingi wa kombe hilo la dunia.

Taifa hilo la Ghuba lilikuwa na makataa ya hadi tarehe 12 Februari 2014 kuifahamisha shirikisho la soka duniani Fifa mikakati ya kuboresha hali ya utendakazi wa wafanyikazi .

Mustakabali huo mpya wa utendakazi wenye ukurasa 50 ,umeundwa kwa ushirikiano wa shirika la wafanyikazi duniani ILO.

Mbali na vifo vya wafanyikazi 185 mwaka uliopita,inaaminika kuwa idadi kubwa ya wafanyikazi wamejeruhiwa kazini kutokana na mazingara mabaya ya kufanyia kazi. Kumeibuka ,pia maswali kuhusiana na makazi duni ya wafanyikazi.

Mashirika ya wafanyikazi na yale ya kupigania haki za kibinadamu yamelalamikia vikali mfumo wa Qatar wa uajiri uitwao ''Kefala '' ambao unapatanisha hati ya usafiri ama VISA na kampuni inayowaajiri mfanyikazi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wafanyakazi Qatar 2022

Mashirika hayo yanasema kuwa mfumo huo unawanyima wafanyikazi haki ya kuondoka Qatar bila ya idhini ya mwajiri wao pindi wanapotofautiana ama kudhulumiwa.

Katibu Mkuu wa kamati andalizi ya qatar 2022 Hassan Al-Thawadi, amesisitiza kuwa mashindano hayo hayatafaidi jasho na damu ya watu.

Hali na haki ya wafanyikazi wanaojenga viwanja vya kombe la dunia vitakavyotumika mwaka wa 2022 ilizua mjadala mwaka uliopita baada ya mashirika ya kupigania haki za wafanyikazi duniani kudai kuwa wenye kandarasi za kujenga viwanja na muundo msingi wa Qatar 2022 walikuwa wamewaajiri raiya wa kigeni ambao walikuwa wanafanyishwa kazi bila malipo ama kwa malipo duni.

Qatar2022Rais wa shirikisho la soka duniani Sepp Blatter aliingilia kati na kuahidi kufanya mashauriano na Kiongozi wa taifa hilo lenya utajiri mkubwa wa mafuta.

Mashindano hayo yameripotiwa kuwa yataigharimu Qatar dola bilioni 200 .