Minala ana umri wa miaka 17-Lazio

Haki miliki ya picha Joseph Minala
Image caption Joseph minala

Klabu ya Lazio imesisitiza kuwa mmoja ya wachezaji wao-Joseph Minala wa Cameroon ana umri wa miaka kumi na saba kama alivyosema baada ya ripoti kusambazwa kuwa ana miaka arobaini na moja.

Klabu hiyo imesema kuwa cheti cha kuzaliwa cha mchezaji huyo kilikuwa halali.

Minala, ambaye ameshiriki katika mashindano ya vijana chipukizi katika klabu hiyo, pia alitoa taarifa akikana madai kuwa aliliambia mtandao moja wa Kiafrika kuwa alikuwa amedanganya umri wake.

Sakata hiyo sasa huenda ikahujumu mchezo wa Minala ambao katika miezi ya hivi karibuni imekuwa ikiimarika na huenda akakosa fursa ya kujiunga na vilabu vingine endapo mzozo huo utaendelea.

Shirikisho la mchezo wa soka nchini Italia, halijasema lolote kuhusu suala hilo sawai na shirikisho la mchezo wa soka nchini Cameroon.

Katika miaka ya hivi karibuni wachezaji wengi wa Kiafrika wameshutumiwa kwa kudanganya umri wao ili kushiriki ligi ya vijana chipukizi ili kuimarisha nafasi yao ya kujiunga na vilabu vya ulaya.