Arsenal yalipiza kisasi Liverpool

Image caption Arsenal ikichuana na Liverpool

Arsenal iliishinda Liverpool mabao mawili kwa moja na kufuzu kushiriki katika robo fainali ya mchuano wa FA.

Ushindi huo umekuwa na umuhimu mkubwa kwa Arsenal na kuirejeshea matuamini baada ya kushindwa huko Anfield mabao 5-1 katika mechi ya ligi kuu ya Uingereza.

Alex Oxlade- Chamberlain alitia kimiani bao la kwanza katika dakika ya 16 ya kipindi cha kwanza .

Kiungo huyo wa Uingereza alichangia bao la pili mapema katika kipindi cha pili alipomvurumishia pasi safi Lukas Podolski na kufanya mambo kuwa 2-0 kufikia dakika ya 47 ya mechi hiyo iliyokuwa sawa na marudio ya mechi ya ligi kuu ya premia wiki iliyopita .

Haki miliki ya picha PA
Image caption Kocha Arsene Wenger

Kinyume na ilivyokuwa wakati huo safu ya ulinzi ya Arsenal ikivuja mabao matano safu hiyo ilikuwa dhabiti na kuinyima Liverpool fursa ya kuliona lango lao.

Safu ya ulinzi ya Arsenal ilistahimilia Wimbi baada ya wimbi ya mashambulizi ya Liverpool .

Hata hivyo juhudi zao zilizaa matunda nahodha Steven Gerrard alipofunga bao la kufutia machozi la Liverpool kwa mkwaju wa penalty dakika 14 baadaye.

Ushindi huo uliwapa motisha Arsenal wanaoialika Bayern Munich Jumatano wiki hii katika mchuano wa klabu bingwa barani Ulaya.

Meneja wa Arsenal , Arsen Wenger, amesema kwamba timu yake ilfuata maagizo yake kikamilifu ili kutwaa ushindi huo.

Katika matokeo mengine , Everton iliilaza Swansea 3-1 huku Shefield United ikairamba Nottingham Forest 3-1.