Spurs yalaumu uwanja Ukraine

Yafungwa Tottenham yalaumu uwanja kwa kichapo.

Kocha mkuu wa Tottenham hotspurs ya Uingereza, Tim Sherwood amesema uwanja wa FC Dnipro ya Ukraine haufai kabisa.

Sherwood alilaumu uwanja huo kwa kichapo cha bao moja kwa nunge katika mraundi ya kwanza ya mchuano wa ligi ya Europa huko Ukraine.

Spurs ilishindwa mechi yake ya kwanza baada ya kucheza mechi 16.

Hata hivyo, Spurs itajilaumu yenyewe kwa kushindwa kufunga mabao fursa yao nzuri ikipotezwa na Roberto Soldado.

Nacer Chadli naye hakutumia vyema fursa aliyopata lakini kama mbaazi aliyekosa kuzaa na kulaumu jua, Sherwood anasingizia uwanja huo wa Ukraine.

Kutokana na kichapo hicho sasa Tottenham italazimika kufanya kazi ya ziada tarehe 27 Februari katika mkondo wa pili timu hizo zitakapokwaruzana ilikufufua matumaini yake ya kusonga mbele kwenye mkondo robo fainali.

Dnipro ilisajili ushindi muhimu nyumbani kupitia bao la Yevhen Konoplyanka kwa njia ya penalti.

Ushindi huo muhimu kwa aliyekuwa kocha wa Spurs Juande Ramos, inawahakikishia afueni watakapozuru Uingereza mwishoni mwa mwezi huu.

Spurs ilikuwa na rekodi ya kufunga mabao 23 katika mechi nane za ligi ya Europa .Hii ndiyo iliyokuwa mara ya kwanza timu hiyo kushindwa kufunga baoo katika mechi ya ligi hiyo ya daraja la pili barani ulaya.