Yanga kupepetana na Al-Ahly

Haki miliki ya picha Yanga
Image caption Kikosi cha Young Africans ya Tanzania

Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Mabingwa barani Afrika, Young Africans, maarufu kama "Yanga" leo hii wanakabiliana na mabingwa watetezi wa kombe hilo, Al-Ahly ya Misri katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kuingia katika hatua ya raundi ya kwanza ya michuano hii, Yanga waliitupa nje timu ya Comorro, Komorozine kwa kuichabanga jumla ya magoli 12-2. Katika mchezo wa kwanza na Komorozine, uliofanyika jijini Dar es Saalm,Yanga iliitwisha mzigo wa magoli 7-0 na kuiadhibu tena nyumbani kwao Comorro mabao 5-2, hivyo kujikuta katika raudni ya kwanza ikipangiwa kukutana na al-Ahly.

Yanga imekuwa na msukumo mkubwa wa kupata ushindi baada ya mwenendo wake wa kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa na ligi kuu ya nyumbani. Katika mapambano yaliyopita kati ya Yanga na Al-Ahly, daima timu hiyo ya Misri imekuwa ikiibuka mbabe kwa kuifunga na kuitoa Yanga katika mashindano kama hayo kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, mthalani mwaka 2009, katika hatua kama hii Yanga ilichapwa na al-ahly mabao 4-0 na kutolewa nje.

Haki miliki ya picha s
Image caption Wachezaji wa timu ya al-Ahly ya Misri

Hata hivyo, safari hii, Yanga imeonekana kupania kusonga mbele katika michuano hiyo ya Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF, kwani imefanya maandalizi makubwa ikiwemo kupiga kambi ya wiki mbili nchini Uturuki, barani Ulaya na kuendelea kufanya vizuri katika ligi kuu ya nyumbani.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans Pluijn anajivunia kikosi chake na kutamba kwamba safari hii, al-Ahly hawatatoka salama katika Uwanja wa Taifa, akijigamba kwamba atawafunga kwani anazifahamu vizuri mbinu za timu hiyo.

Mechi nyingine zitakazochezwa leo za mabingwa wa kombe la Afrika ni Gor Mahia ya Kenya watakuwa wenyeji wa EST ya Tunisia, Kampala City Council ya Uganda itasafiri kwenda Zambia kumenyana na Nkana Red Devil.