Yanga yaiduwaza Al-Ahly 1-0

Image caption Kikosi cha Yanga kilichoilaza Al-Alhly 1-0

Mabingwa wa soka Tanzania bara,klabu ya Yanga ya Dar es Salaa,imefanikiwa kuuvunja mwiko wa kutozifunga timu kutoka Misri baada ya kuilaza National Al Ahly bao 1-0 hapo jana kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam katika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika.

Katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na maelfu ya mashabiki kutoka kila pembe ya jiji la Dar es Salaam,wengine wakitoka mikoani,Yanga ilipata bao hilo pekee na la ushindi katika dakika ya 83 kufuatia mpira wa kona iliyopigwa na Simon Msuva iliyounganishwa kwa kichwa cha nguvu na Mlinzi na nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub almaaruf Canavaro.

Ingawa ki mpira ni ushindi mwembamba lakini kwa upande wa Yanga mara ya kwanza kwa Mabingwa hao wa Tanzania kuifunga timu hiyo ya Misri ambayo mbali na kuwa mabingwa watetezi lakini pia ndio klabu bora na yenye mafanikio kuliko klabu yoyote barani Afrika ambayo kwa miaka mingi imekuwa imekuwa inazitesa klabu za Tanzania hasa Yanga ambayo mwaka 1982 iliwahi kuifunga bao 5-0 katika mechiy a awali jijini Cairo kabla ya kwenda sare ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo Yanga imejiweka mazingira mazuri kufuzu huku ikihitaji sare ya namna yoyote katika mechi ya marudiano itakayopigwa jijini Cairo Jumapili ijayo tarehe 9 mwezi huu wa March.

Haki miliki ya picha s
Image caption Kikosi cha al-Ahly ya Misri

Mabingwa hao wa Tanzania ndio wawakilishi pekee waliobaki kwenye michuano ya kimataifa mwaka huu, baada ya Azam kutolewa na Feroviario ya Msumbiji kwa bao 2-1 katika michuano ya kuwania kombe la shirikisho la soka barani Afrika CAF,katika raundi ya kwanza.

Yanga inapaswa kujizatiti ili kuweza kujiwekea historia barani Afrika iwapo itafanikiwa kuivua Ubingwa National Al Ahly kama ilivyowahi kutokea kwa Simba mwaka 2003 ilipofanikiwa kuivua ubingwa Zamalek pia ya Misri ambao ni wapinzani wa Al Ahly kwa mikwaju ya Penalti.

Kwa upande mwingine matokeo hayo ya Yanga, imekuwa ahueni kubwa kwa klabu za soka katika ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Gor Mahia ya Kenya kulazwa bao 3-2 nyumbani mjini Nairobi na Esperance ya Tunisia huku KCC ya Uganda ikitoka sare ya 2-2 ugenini mjini Kitwe Zambia, dhidi ya Nkana Red Devils.

Michezo mingine ya Jumamosi ni Flambeau de l'Est ya Burundi imefanikiwa kuicharaza Coton Sport ya Cameroun 1-0, Zamaleck ya Misri waliwakaribisha Kabuscorp ya Angola na kuwalaza 1-0, huku Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ikipata ushindi mnono wa magoli 4-0 dhidi ya Liga Muculmana ya Msumbiji.